Jumapili, Juni 13, 2021
Ndugu zangu wapendwa, katika masomo yetu ya leo, tunasikia juu ya tamaa ya mwanadamu kuupata ufalme wa Amani na utulivu. Somo la kwanza, linatabiri ujio wa ufalme huu na unabii huu ulitimia kwa ujio wa Yesu duniani na katika injili Yesu anatangaza tabia za ufalme huu. Tutaona kwamba, ingawa ufalme huu ni mpana kuliko kanisa, kanisa ndio kielelezo cha ufalme huu na katika kuujenga ufalme huu, sisi lazima kuwa mstari wa mbele. Huu ndio ujumbe ninaowaomba tuutafakari kwa pamoja.
Tukianza kwa kuziangalia nyimbo zetu kuu za leo, wimbo wa mwanzo unatoka katika zaburi ya 27. Hii ni zaburi aliyoiimba Daudi akiomba usalama toka kwa Mungu dhidi ya maadui zake. Yeye alikabiliwa na maadui wakubwa wa tatu enzi za uhai wake: Goliath, Sauli na Absalaom. Hivyo, anamlilia Mungu na kumwambia ee Mungu, tafadhali usiniache kabisa, angalia maadui wangu ni wengi. Ni mwaliko kwetu pia kumlilia Mungu siku ya leo.
Zaburi ya wimbo wa katikati inatoka zaburi ya 91. Hii ni zaburi ya shukrani iliyotungwa na walawi waliohudumu hekaluni na ilitumika katika siku ya sabato kumshukuru Mungu aliyewawezesha kuishi wiki nzima salama na kusali pamoja na kupata usalama wa kutosha. Ni mwaliko kwetu na sisi leo tunapoiimba zaburi hii, nasi tuwe kama hawa walawi: leo ni sabato yetu, hivyo tumshukuru Mungu kwa kiuhakika aliyetupatia siku hii nzuri na hivyo kweli mshukuru. Katutendea makubwa sana kwa wiki nzima.
Tukianza kwa kuliangalia somo la kwanza, hapa tunakutana na nabii Ezekieli akihubiri baada ya ule uhamisho wa kwanza wa wana wa Yuda mwaka 597BC. Katika uhamisho huu, waliohamishwa ni wale watu maarufu, waliokuwa na vyeo na wasomi na wafanyabiashara pamoja na mfalme Jehoiakin. Ingawa Ezekiel aliwaambia waziwazi kwamba dhambi zao ndizo zilizosababisha yote haya, pia aliwaeleza kwamba Mungu hatawaacha milele. Upo wakati atakapowajia watu wake na kuwaokoa utumwani.
Katika somo letu la kwanza leo, yeye anatoa unabii ulioshiba matumani: anasema “Bwana Mungu atakitwaa kilele kirefu cha mwerezi na kukipandikiza mahali pake; na katika vitawi vyake vilivyojuu atatwaa katawi kimoja chororo na kukipanda juu ya mlima ulioinuka sana-na haka katawi katakua na kuwa mwerezi maarufu sana, katazaa sana, na ndege wote watakuja kutafuta malisho chini yake na miti yote ya mashambani itaushangaa ukubwa wake na kuukiri uwezo wa Bwana aliyefanya yote haya.
Ndugu zangu, hapa nabii anatumia lugha ya picha: Mwerezi ni shina lote la ufalme wa Daudi. Katika Ezekiel 17:3, Mfalme Nebuchadnezer anaelezewa na nabii Ezekiel kama mwewe au tai mwenye nguvu aliyeruka na kutua juu ya mwerezi uliopo juu ya milima ya Yerusalem na kukwanyua tawi la juu kabisa la mwerezi huu na kulihamishia Babuloni. Hili tawi la juu kabisa linamwakilisha mfalme wa Yuda aliyeitwa Jehoiakini. Yeye katika mwaka 597BC, alitekwa na mfalme Nebuchadnezer na kupelekwa utumwani Babuloni.
Nebukadneza alimchagua kijana mmoja aitwaye Zedekia awe mfalme kibaraka juu ya Yuda. Yeye aliowaongoza watu katika dhambi. Alimtesa sana nabii Yeremia na alikwenda kufanya mkataba na Wamisri na kuliletea taifa la Yuda madhara mengi. Mfalme Nebuchadnezer aliivamia Yuda kwa mara ya pili mwaka 587BC na kuiteketeza Yerusalem na hekalu na kuipeleka idadi kubwa ya watu uhamishoni.
Leo Mungu anakiri kutokuiacha Yuda. Anaahidi kukitwaa katawi cha juu chororo-toka juu ya mwerezi na kukapandikiza juu ya kilele cha juu ya milima ya Yerusalemu: haka katawi katakua na kuwa mwerezi wenye ukuu wa ajabu mbele ya mataifa yote. Huu mwerezi utailetea dunia raha kwani wanadamu watakuja kutafuta malisho na usalama chini ya matawi yake. Hii itaifanya miti yote ya dunia, yaani wafalme wote wa Dunia, wautambue ukuu wa Bwana Mungu wa Israeli.
Unabii wa maneno haya ulitimia kwa mapana Zaidi kwa ujio wa Kristo. Yeye kweli alikuwa katawi chororo toka shina la Daudi na amekuwa kimbilio la vizazi vyote. Yeye alikuja kuutangaza ufalme wa Mungu na katika injili yetu ya leo anaelezea kwa mifano tabia za ufalme wa Mungu aliokuja kuutangaza.
Mfano wa kwanza: anasema kwamba ufalme huu ni kama mkulima aoteshaye mbegu na baada ya hapa-huota yenyewe. Hapa anamaanisha kwamba ufalme aliokuja kuutangaza utakua wenyewe bila fujo. Hautahitaji vitu kama vita au mapinduzi au wanasiasa au wasomi au wanafalsafa maarufu au wanajeshi maarufu kama akina Alexander the Great au Joseph Stalin au watu wakorofi ili wausaidie ukue. Utaanza kidogokidogo lakini mwishowe kila mmoja atatamani kupata ulinzi chini yake. Na kitakachowezesha yote haya ni Roho wa Bwana aliyendani ya ufalme huu, ndiye atakayeuwezesha ukue usiku na mchana.
Tabia ya pili ya ufalme huu inafananishwa na chembe ndogo ya haradali ambayo baada ya kukua, mti wake huonyesha ukubwa wa ajabu ukilinganisha na udogo wa mbegu yake. Ni kama maboga makubwa yanavyoanzia kwenye vishina vidogo vidogo. Hii yamaanisha kwamba ufalme huu ulikuwa umejificha ndani yake yeye: mtu anayeonekana kuwa dhaifu na fukara lakini ndani alibeba makuu.
Kipindi hiki, Wayahudi walitamani sana atokee kiongozi atakayepindua utawala wa Warumi waliokuwa wanawatawala na hivyo Yesu alikataa watu kumhusisha na malengo ya kutaka kupindua na ndio sababu za kutumia mifano ya kiupole kama hii.
Ndugu zangu, ingawa ufalme uliotangazwa na Kristo ni mpana kuliko kanisa, kanisa ni kielelezo cha ufalme huu na ndilo linaloshikilia ukamilifu wa nyezo zote za kumpeleka mtu kwenye ufalme huu (LG 1).
Kanisa lilianza katika hali ya kinyonge kabisa: Yesu hakulianzisha mikononi mwa watu maarufu-wasomi walikuja baadaye: viongozi wake walikuwa wavuvi, wakulima, wafugaji na watoza ushuru. Pia halikuhitaji wanafalsafa maarufu ili liweze kuhubiri injili. Injili iliyohubiriwa na mvuvi asiyekwenda shule ndiyo iliyomshawishi mwanafalsafa kujiunga na kanisa. Hii yote ni kwa sababu Roho alikuwa ndani ya kanisa akilisaida likue. Na hivyo liliweza kuwagusa watu wengi ajabu. Hadi leo, mawazo ya injili, yameiletea dunia faida kubwa ajabu. Na ndio yanayokimbiliwa kila patokeapo vita, chuki, au unyanyasaji, au unyonyaji au ukandamizaji. Haya yanategemewa sana kuiletea dunia amani.
Hata wahubiri wa dini mbalimbali wamebadilishwa mitazamo yao na injili. Kanisa limetoa mchango mkubwa sana kwa jamii.
Hivyo, tumshukuru Mungu kwa kutufanya kuwa wanachama katika kanisa lake. Hivyo, tusaidie kukuza ufalme wa Mungu. Kila tutendapo tendo jema, tunasaidia kukuza ufalme huu na kulisaidia kanisa kuumulika ulimwengu na kuwavuta wengi chini ya mabawa yake, chini ya mafundisho yake. Hivyo tujitahidi kutenda mema.
Hata kama wewe mgumu kiasi gani, lakini wakati mwingine tenda tu wema ndugu yangu, jua kwamba unahitajika kwa ajili ya kanisa, na wewe kama mkristo-msaiidie Kristo awe mwanga.
Pili, tushirikiane na kanisa kukuza ufalme huu. Ufalme huu unapaswa uoneka kwenye idadi ya watu wanaokuja kutaka faraja toka kwako wewe. Ni wangapi wanaokujaga kukaa chini ya mabawa yako. Kwenye mabawa yako kuna mwiba au upendo au marashi ya kuvutia? Jamani, tujitahidi jamani. Tuvutie watu,tunaongea lugha mbaya tuache. Tutumie sakramenti zake vyema kabisa. Hivyo, tushirikiane na huyu roho, tupokee sakramenti zake vyema, tutoe mchango wetu wa kutosha wa kusaidia Mungu aeneze ufalme wake, dunia iwe na Amani. Hivyo, sehemu ya mchango wangu ni kubwa. Nijitahdii.
Halafu, kanisa lisijishikishe na watu Fulani Fulani kwamba ati ndio litakua. Tumesikia kwamba Roho ndiye anayesaidia ukuaji wa huu ufalme. Kuna kasumba labda kwa kanisa kushikamana na watu Fulani Fulani, ndio litaweza kukua. Hapana! Sio, wanasiasa, wanafalsafa-sawa wanaweza kulichangia kanisa mchango wao lakini bila hata mchango wao, linakwenda. Hivyo, tuache kujishikisha na class ya watu Fulani, au mapadre kwenda kwa familia hii tu. Hapana, jua kwamba kanisa lilikuwako kabla ya kupata mtu yeyote mwenye nguvu. Mtu wa kwanza alikuwa mvuvi maskini. Hivyo, acha kabisa.
Ufalme wa Mungu ni wa Amani na utulivu. Jua kwamba unapokabidhiwa cheo, hapa kanisani, kamwe usikitumie kwenye kuonyeshea ubabe wako. Yaani huruma inabidi itawale ajabu. Ubabe sio kwenye institutions za kanisa. Hata kama wewe ni mwenyekiti-ukiwa unaongoza cheo chochote kanisani, jua kwamba ukishaweka ubabe, basi wewe sio wa Mungu tena. Waswahili wanasema mechemka.
Mtakatifu Paulo katika somo la pili anatuambia kwamba kila mmoja wetu atajongea kiti cha hukumu na kupokea stahili yake. Hii siku kwa wengi wetu itakuwa ya fedheha kwani wengi wetu huwa tunaficha dhambi; na hata tunapoungama, kuna upande ambao huwa hatuugusi-tunataka mtu asiutambue- kwani kuusema upande huu, inahitaji ujasiri na ukishaweza kuusema, basi maisha yetu hubadilika. Na pale upande huu utagundulika kwa wengine kwa bila ya sisi kutaka, hapa ndipo tunapoishiwa nguvu.
Mfano: ni pale tunapojichanganya na kutuma sms au picha tusiyoitaka ijulikane kwa group tusilodhamiria. Hapa ndipo utakaposhuhudia jinsi tunapoanza kujitetea kwa presha kali kabisa na kusema uongo.
Hivyo, tujitahidi ndugu zangu. Tusikubali kutambulishwa na sifa mbaya kama ulevi, dharau na dhuluma. Mfano, nilikwenda kijijini nikakutana na wale vijana vilivyokuwa vitoto, vilivyotunzwa na ile jamii, vikalishwa navyo maparachichi, vile vilivyokuwa haviwezi hata kuvaa-jamii ilivilisha na vile vilikuwa haviwezi hata kupenga kamasi.
Lakini ukienda sasa hivi, unakuta ati baadhi ndio vinatesa wale wazee. Baadhi vimekuwa wezi na usiku vinakuja na panga au sime kuwatesa wale wazee waliowatunza kuwaambia toeni pesa. Jamani! Hii laana tutapeleka wapi? Tuache tabia hizi jamani.
Tusikubali kutambulishwa na sifa mbaya hivi. Tubadilike.
Jukumu letu ni la kuutangaza ufalme wa Mungu kwa kutenda mema ili wengi waje na kupata faraja chini yetu. Kristo ni mwanga wa ulimwengu na mwanga huo huchomoza kupitia kanisa. Nasi tuwe mwanga kwa jamii yetu. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Sephrian Angelo
Shukrani kwa tafakari nzuri sana. Tumebakiwa sana kupitia tafakari hiiIngia utoe maoni