Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Juni 14, 2021

Jumatatu, Juni 14, 2021.
Juma la 11 la Mwaka
2 Kor 6: 1-10;
Zab 98: 1-4;
Mt 5: 38-42

KUUSHINDA UOVU KWA WEMA!

Ndugu zangu, karibuni sana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika neno la Bwana katika somo la kwanza, Mt. Paulo anawasisitizia Wakristo wa Korintho kwamba wakati uliokubalika ndio sasa, na saa ya wokovu ndio sasa. Hivyo Mwenyezi Mungu yupo tayari kutusaidia wakati huu, na yupo tayari kutupa wakovu kwa wakati huu.
Hivyo Paulo anawasihi Wakristo wa Wakorintho kwamba wasiwe watu wa kusubirisha mambo, au kudhania kwamba maisha mema wataanza kuyaishi kesho, au wataanza kusali kesho. Anawasihi wafanye mambo yote mema kwa sasa, kwani siku ya wokovu ni sasa na wakati ndio huu. Anawasihi waepuke maisha yenye kuwakwaza wenzao-wahakikishe kwamba wanajipatia sifa njema. Hivyo katika maisha yao wazishidishe uvumilivu, upendo usio na unafiki, hata wakinenwa waendelee kuwa na uvumilivu. Mungu atawasaidia.
Naomba neno hili toka kwa Paulo litufariji na sisi pia ndugu zangu. Saa ya wokuvu kwetu ni sasa. Tumeshuhudia wenzetu wakipata vifo vya gafla na kututoka bila hata ya sisi kutarajia. Sisi tutambue kwamba saa ya wokovu ndio sasa. Hivyo tuwe watu wa kujiandaa, tuishi maisha mema. Tuzidishe na Roho ya uvumilivu. Mwenyezi Mungu atusaidie. Pia tuondoe aina yoyote ile ya majivuno kati yetu na kutawaliwa na tamaa za mwili. Saa ya wokovu ndio sasa.
Yesu katika Injili anawaeleza wafuasi wake kwamba tusishindane na mtu mwovu. Watu waovu ni watu wenye hila. Wanajua kutengeneza fitina. Kwa kuwa kazi zao ni kutenda uovu, watakuwa tayari kutengeneza kila aina ya hila ili kutuangusha. Wapo watakaokuwa tayari hata kuutoa uhai wako. Tumeshuhudia baadhi ya watu waovu wakitoa fedha ili waangamize wapinzani wao.
Yesu leo anatueleza kwamba tusishindane na watu kama hawa. Kitakachowaaibisha ni wema wetu. Wakitenda uovu na sisi tukiepuka kushindana nao, wataona aibu, watakosa mtu wa kuanzisha naye visa na mwishowe wataona aibu na kukimbia. Namna hii tutaweza kushinda uovu kwa wema. Maneno haya yatutie moyo hasa kwa baadhi yetu tunaoishi na majirani au wafanyakazi au wenzetu waovu. Wapo watu waovu kweli. Lakini kitakachowabadilisha watu kama hawa sio uovu, au lugha mbaya au vifungo vya gerezani. Watu waovu mara nyingi wanatafuta mtu mwovu mwingine wa kushindana naye. Hivyo atakapokutana na mtu mwema, atakaposhindwa kupata wa kushindana naye, hapo ataona aibu tu na kukimbia.
Sisi tusiache kuwa watu wema ndugu zangu. kwa wema wetu, tutaibadili dunia. Lakini kwa ubabe na kwa kutoa adhabu kali dunia itazidi kuwa ovu.

Maoni


Ingia utoe maoni