Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Juni 07, 2021

Jumatatu, Juni 7, 2021.
Juma la 10 la Mwaka

2 Kor 1: 1-7;
Zab 34: 2-9;
Mt 5: 1-12


HERI WALIO…..!
Karibuni sana ndugu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria mama wa Kanisa. Ni kumbukumbu iliyoamriwa iadhimishwe baada ya Pentecoste kuonesha ushirika na mchango wa Maria katika Kanisa.
Roho Mtakatifu aliwashukia mitume na wafuasi wa kwanza wa Kristo siku ya Pentecoste. Roho Mtakatifu alikuwa na mchango mkubwa sana katika kuiunda, kuiongoza na kuilinda hii jamii ya Mwanzo ya Wakristo. Roho aliwaondolea woga, aliwafanya watoke na kwenda kuhubiri injili kila mahali. Tukisoma katika Matendo ya Mitume 2:41, tunagundua kwamba kwa nguvu ya Roho, karibu watu elfu tatu waliweza kubatizwa katika ile siku ya Pentecoste. Hakika Roho alitoa nguvu ya ajabu. Roho alizidi kuwaongoza, kuwatetea na kulifundisha kanisa.
Roho Mtakatifu amelitetea kanisa ili lisiangamizwe na Makaisari wakorofi kama akina Nero na Domitian. Roho Mtakatifu ndiye mwenye kulitakasa kanisa na kulifanya kuwa Israeli mpya na kwa njia yake tunaweza kumfikia Mwenyezi Mungu wetu-bila Roho Mtakatifu, kanisa lisingeliweza kuanza na kuwashinda maadui wake.
Mama Maria ni mwenye nafasi kubwa ndani ya kanisa, ndiye aliyekuwa kiongozi na mshauri wa jamii ya kwanza ya Wakristo. Pia amekuwa mwombezi wa kanisa baada ya kupalizwa mbinguni. Nafasi ya Mama Maria katika kanisa ni kubwa sana. Hivyo astahili nafasi ya pekee katika kanisa. Hivyo tunayo kila sababu ya kumheshimu Maria kama Mama wa kanisa baada ya Pentecoste.
Katika somo la kwanza leo, tunasikia juu ya dhambi na uadui uliongia ulimwenguni baada ya dhambi ya Eva. Eva alionesha ukaidi, hakutii sauti ya Mungu na hivyo kuiletea dunia madhara makubwa. Mama Maria alionesha utii mkubwa na kwa utii wake aliiletea dunia ukombozi. Na leo anachaguliwa na Mwanae kuwa Mama wa Wafuasi wake. Mama Maria aliweza yote haya kwa sababu alionesha utii mkubwa. Kama angeonesha ukaidi, hakika asingaliweza kuwa wa faida kwetu.
Utii huu wa Mama Maria ututie moyo na sisi tupate kuwa watii. Utii utatuletea faida kubwa. Pia utusaidie sisi kukimbilia ulinzi wa Mama Maria kila siku. Kanisa lisimtupe Mama Maria pembeni kwa wakati wowote. Mama Maria ndiye mwombezi wake. Likimbilie msaada na maombezi yake kwa kila siku.

Maoni


Ingia utoe maoni