Jumatatu, Mei 31, 2021
Jumatatu, Mei 31, 2021
Juma la 9 la Mwaka B wa Kanisa
SIKUKUU YA BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI
SOMO 1 Sef. 3:14-18 au Rum. 12:9-16
Isa. 12:2-6 (K) 6
INJILI Lk. 1:39-56
Anafurahi na kushangilia.
Karibuni ndugu zangu katika tafakari yetu ya siku hii ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo tunaadhimisha siku ya maamkio ya Bikira Maria. Tunakumbuka ile siku ambapo Mama Maria alikwenda kumwamkia na kumfariji shangazi yake Elizabethi. Hili lilikuwa ni tukio la kinyenyekevu kwani Maria aliyekuwa Mama na cheo cha kuitwa Mama wa Mungu, alipata kumsalimia Mama yake Yohane Mbatizaji ambaye yeye alikuwa ni Mama wa mtumishi atakayemtangulia Yesu, akiwaonyesha watu namna ya kujiandaa ili kumpokea Yesu.
Tukio hili ni mfano mkubwa kwetu wa kuigwa kwani kwa kawaida katika jamii zetu, anayetembelea wengine ni yule mdogo; mwenye shida, watu wazito, wenye pesa zao, na raha zao huwa hawatembeleagi wengine mara nyingi; lakini tukio hili ni kinyume. Hivyo lazima liigwe na liwe kwetu mfano. Hata Elizabethi mwenyewe anashangaa na kusema inakuwaje hili Mama wa Bwana wangu kunitembelea? Na hata Yohane anafurahi na kushangilia.
Na hapa twajifunza unyenyekevu wa Mungu kwamba ni Mungu mwenyewe ambaye huja ili kututafuta na sio vinginevyo. Yeye anazunguka akitutafuta. Hivyo mpokee kwa furaha kama Yohane Mbatizaji anavyompokea Yesu leo, kama Elizabethi anavyompokea Maria leo. Huu ndio ukuu wa hii siku ndugu zangu.
Tukijaribu kuyaangalia masomo yetu kuhusu siku hii, somo la kwanza linatoka katika waraka wa mtume Paulo kwa Warumi. Hapa tunakuna na Paulo akiwafundisha wale wakristo wa Roma kwamba wanapaswa kuishi na wenzao vyema. Wachukie jambo baya, wapendane kidugu, kila mmoja amfikirie mwenzake kwa heshima, tumaini lao kwa Bwana liwaweke daima wawe na furaha. Anawaeleza pia wafurahi na wenye kufurahi na kulia na wale wenye kulia. Tunaweza kusema katika somo hili, Paulo anawataka hawa wakristo wa Roma wawe na Roho na moyo kama wa Bikira Maria anavyokwenda kumtembelea Elizabethi leo.
Wengi walioongokea ukristo katika kanisa hili la Roma ni wale waliokuwa na uwezo wa chini. Pia walikuwa wanatengwa na baadhi ya wanafamilia wao kwa tendo lao hili la kuongokea ukristo. Hivyo wengi waliishi katika maisha ya shida. Kwa kweli walihitaji kufarijiwa na wakristo wenzao. Wakristo wenzao ndio wangetakiwa sasa wawe ndio Baba na Mama zao, wawe ndio ndugu zao. Na kwa kweli lile kanisa la mwanzo lilifanikiwa sana kwa sababu baada ya mtu kutengwa na ndugu zake kwa sababu ya kuuongokea ukristo, waliobakia kama ndugu kwake ni wale wakristo wenzake. Wale wakristo walikutana, wakasaidiana, wakatiana moyo kwenye shida zao, wakatembeleana nyumbani mwao, wakasali pamoja, wakalea watoto wao pamoja na kwa kufanya hivi waliweza kumshinda adui kirahisi.
Katika injili tunagundua kwamba kumbe ukristo tangu mwanzo ulipaswa uwe na hali za namna hizi. Ulipaswa uwe wa kusaidiana na kutiana moyo na hapa katika injili tunamuona Maria akienda kumtia moyo shangazi yake Elizabethi.
Ndugu zangu, siku hii ya leo na masomo yetu ya leo yatutie moyo ili hasa tupate kuwafikia wenzetu. Halafu kwenye kuwafikia wenzetu, haimaanishi ni yule mwenye shida tu anapaswa kumtembelea mkubwa, au maskini anapaswa kwenda kumtembelea boss, wewe bossi unaalikwa kama Mama Maria leo kuwatembelea wafanyakazi wako au maskini wako. Kingine ni kwamba kuna baadhi yetu, tena wa kutoka familia moja, ambao hatusaidiani. Unakuta mwanafamilia mmoja anateseka, watoto wake hawawezi hata kulipa kodi lakini unakuta shangazi au mjomba wa hawa watoto ana uwezo wa kutosha na hawawasaidii. Tuache tabia hizi ndugu zangu. Tusaidie wenzetu; ubinafsi tuache. Hautatufikisha popote ndugu zangu. Bikira Maria awe kwetu kioo na mwombezi.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni