Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Mei 10, 2021

Jumatatu, Mei 10 2021.
Juma la 6 la Pasaka

Mdo 16: 11-15;
Zab 149: 1-6, 9;
Yn 15:26 - 16:4.

ROHO MTAKATIFU: MSAIDIZI
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Tafakari yetu ya neno la Bwana inaanza kwa kuliangalia somo la injili. Somo hili lasisitizia juu ya ujio wa msaidizi yaani Roho Mtakatifu. Yeye aliahidiwa kuja kusaidia katika changamoto mbalimbali za wafuasi wa Yesu.
Yesu anawatabiria wanafunzi wake kwamba upo wakati ambapo watakumbana na upinzani mkubwa sana na kuchukiwa sana na baadhi ya watu-yaani hata kuwauwa itaonekana kana kwamba ni kutenda jambo jema-yaani watu wamewachukia kupita kiasi. Hali hii imekuwa ikitokea ndugu zangu na kuwapata baadhi yetu. Waweza kukutana na mtu anayechukiwa kupita kiasi, anayetangazwa na kusemwa vibaya sana-ukijaribu kuuliza sababu za kuchukiwa hivyo wakati mwingine hupati sababu za msingi. Hakika hatuwezi kuwalazimisha watu watupende au wawapende wenzetu. Tunapaswa kutenda wema-juu ya kutupenda au kutuchukia ni juu yao. Lakini basi tusiache kumkimbilia msaidizi wetu yaani Roho Mtakatifu katika kupambana na chuki za watu kama hawa.
Wana wa Israeli walipokuwa wakisafiri jangwani kuelekea nchi ya ahadi, yalitokea makabila yaliyowaonea wivu na kutaka kuwapiga. Lakini walimkimbilia msaidizi wao, yaani ile nguzo ya moto na hakika walishinda. Nasi tumkimbilie msaidizi wetu yaani Roho Mtakatifu. Wanaotuchukia hakika hawataweza kutushinda.
Tuwaombee pia wale wanaochukia kupita kiasi. Mungu awasaidie.
Katika somo la kwanza, Msaidizi yaani Roho Mtakatifu anaufungua Moyo wa Lydia na kuwapokea kina Paulo. Paulo hakuwa na rafiki alipofika Philip kwa mara ya kwanza. Lakini Roho wa Bwana anaufungua moyo wa Mama Lydia na kumpokea Paulo. Hakika msaidizi amewatendea makubwa kina Paulo-amekuja kuwasaidia. Nasi tusiache kumkimbilia msaidizi wetu.
Tumwombe kila siku, msaidizi wetu yupo. Mkaribishe akusaidie kubeba maumivu yako, abebe pia na changamoto zako na maadui zako wote na akupatie kipato cha kila siku. Akusaidie madeni yasizidi kipato chako. Akupe na uwezo uweze kulipa madeni yako na kuwa na amani.

Maoni


Ingia utoe maoni