Jumamosi, Mei 08, 2021
Jumamosi, Mei 8, 2021.
Juma la 5 la Pasaka
Mdo 16: 1-10;
Zab 100: 1-3,5 (K. 1);
Yn 15: 18-21.
KUKUTANA NA MATESO
Karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu. Tafakari yetu ya neno la Bwana naomba iongozwe na somo letu la kwanza ambapo tunakutana na Paulo akiona maono ya kualikwa na watu wa Makedonia kwa ajili ya kuhubiri habari njema.
Watu wa Makedonia walimhitaji Kristo awaletee faraja maishani mwao. Walihitaji Kristo awaponye magonjwa yao, awaletee uhuru, utulivu na upendo katika jamaa zao. Walitaka kuondokana na ibada kwa miungu na ushirikina na kufurahia uhuru unaopatikana kwa Kristo. Hii ilikuwa hamu yao. Nasi tunaalikwa siku ya leo tuwe na hamu ya namna hii. Kristo tayari amekwishatuletea uhuru, tuukubali uhuru wa namna hii. Wengi wetu tumeshindwa kumfaidi Kristo wetu kwa sababu ya kurudi nyuma tulipotoka, bado tunangangania tamaduni mbovu tulizoziacha na kufikiri kwamba ndani yake ipo faida zaidi. Hili ndilo linaturudisha nyuma zaidi.
Tunafundishwa kumtamani Kristo kama watu wa Mecedonia wanavyomtamani leo.
Katika somo la injili, Yesu anawahatarisha wanafunzi wake juu ya ujio wa chuki-kwamba wapo watakaowachukia. Hata wakati wanatenda jambo jema, wapo watakaowachukia. Yesu anawaeleza kwamba wasishtushwe na jambo kama hili kwani sio mara ya kwanza kwa jambo kama hili kutokea. Hata Yesu mwenyewe walimtendea hivihivi. Alichukiwa kwasababu ya kutenda mema. Yafaa tutambue kwamba duniani kuna wenye roho mbaya, na pia kuwa binadamu walio wagonjwa wa kisaikolojia pia. Wapo wanaopendelea wenzao wateseke, wapo wasiotaka wengine wapate maendeleo na wengine wanataka dunia irudi nyuma. Hivyo, sio wote wanaweza kufurahia wakikuona ukitenda mema.
Fundisho hili linapaswa kututia moyo katika safari ya utume wetu. Tukiona wanaotupinga pinga tujue kwamba baadhi yao pia ni watu wenye udhaifu na kati yao ni wagonjwa. Hivyo, hawapaswi kuruhusiwa waturudishe nyuma. Kuwaruhusu ni kumpatia shetani ushindi. Tusimpatie shetani ushindi wowote ule.
Maoni
Ingia utoe maoni