Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Mei 06, 2021

Alhamisi, Mei 6, 2021
Juma la 5 Lla Pasaka
Mdo 15: 7-21;
Zab 96: 1-3,10 (K. 3);
Yn 15: 9-11.
KUONGEA LUGHA YA MUNGU!

Karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu ya neno la Bwana inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na mitume wakitafakari kwa pamoja namna ya kuwapokea watu wa mataifa katika kanisa.
Katika kuwapokea, wanaamua kuondoa vikwazo visivyo na lazima mbele yao. Lengo lao ni kumtaka Kristo awatakase watu hawa wa mataifa; mitume wangaliruhusu tamaduni za Kiyahudi kuwa kama moja ya vigezo kuingia ukristo, waamini wengi wangalipoteza dira na kushindwa kujua nafasi ya Kristo maishani mwao. Wangaliishia kushika tamaduni za Kiyahudi na kumsahau Kristo. Hili ndilo lengo la mitume walilokuwa nalo juu yetu-kwamba tuweze kumpokea Kristo na mafundisho sahihi yasiyokuwa na waa.
Nasi tukumbatie nia hii ya mitume ndugu zangu. Tujichunguze na kuona ni wapi tuliporuhusu tamaduni zetu mbaya zikatuzuia kumpokea Kristo sawasawa.
Zipo tamaduni zinazoruhusu polygamy, zenye kuabudu mizimu, zenye kuwatenga baadhi ya wanadamu. Tusikubali tamaduni za namna hii ziturudishe nyuma. Tunapaswa kumruhusu Kristo apenye ndani ya tamaduni hizo na kutuletea mabadiliko makuu. Wapo baadhi yetu ambao wameshindwa kumfurahia Kristo kwa sababu ya kukubali kutawaliwa na tamaduni zisizokuwa na maana. Tusikubali tamaduni zetu au desturi zetu ziwe kwa ajili ya kuturudisha nyuma kila siku.
Katika somo la injili, Yesu anatusisitizia juu ya kuzishika amri zake. Amri zake huokoa, ndizo zitakazotutetea tukiwa hapa duniani na hata baadaye tutakapoondoka hapa duniani ndugu zangu na kusimama mbele ya kiti cha hukumu. Amri hizi ndizo zitakazoendelea kututetea. Sisi tuzidi kuzishika amri za Mungu na hakika hatutashindwa kumsifu Kristo wetu na kumkaribisha abadili maisha yetu.
Amri za Mungu zitatutetea hapa duniani na mbinguni. Duniani tunanyanyasika kwa sababu hatuzitii amri zake. Sisi tuzitii amri za Mungu na hakika tutaishi kwa kujiaamini zaidi. Maisha yenye aibu ni maisha yasiyofuata amri za Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni