Ijumaa, Mei 07, 2021
Ijumaa, Mei 7, 2021
Juma la 5 la Pasaka
Mdo 15: 22-31;
Zab 57: 8-12 (K. 10);
Yn 15: 12-17.
TUMECHAGULIWA KUWA WA MUNGU!
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo linaanza kwa kuliangalia somo la injili ambapo tunakutana na sehemu ya wosia aliouacha Yesu kwa wanafunzi wake kabla ya kuteswa na kifo chake. Anawaagiza kwamba anawapatia amri ya mapendo. Anawaeleza kwamba wasichoke kuwapenda wenzao, hata ikifikia hatua ya kutoa uhai wao kwa ajili ya wenzao.
Yesu anasisitizia hili akijua kwamba hili ndilo litakaloipatia dunia Amani-na ukichoka kupenda hakika hutakaa uweze kumpenda mtu duniani kwani tutakutana na wengine ambao utawaonesha upendo lakini wao hawatajali bali watakutukana. Bila kuwa na bidii katika kupenda, hakika tutakata tamaa tu. Hivyo Yesu anataka tuongeze bidii katika kupenda. Ukweli ni kwamba hadi sasa ni wanadamu wachache walio na utayari wa kuonesha upendo mkuu kiasi hiki.
Kwa mfano, mama anayekubali kufanyiwa upasuaji ili mtoto wake apone ni moja ya eneo ambapo upendo huu unaoneshwa. Pia tumesikia ndugu wakiwachangia wenzao damu na viungo kama figo. Hii ni moja ya maeneo upendo huu unaoneshwa. Lakini pia tutambue kwamba wengi wetu hatujawa tayari kutoka nje ya familia na kuwapenda hata tusiozaliwa nao tumbo moja. Bado tuna tabia ya kuwaonea kinyaa wengine, hasa wale tusiozaliwa nao familia moja. Tumwombe Mungu atuepushe na hali kama hizi. Huyu ni shetani anayetuzuia tushindwe kuwakaribia wenzetu. Tupambane na hali ya kuoneana kinyaa na kujiona sisi wa muhimu sana.
Katika somo la kwanza, mitume baada ya kumaliza kikao chao kuhusu kuwapokea watu wa mataifa katika kanisa, wanatoa tamko na hati rasmi leo. Mafundisho ya hati hii yanasisitiza juu ya upendo. Hati hii inawashauri waepukane na mafundisho na matendo ya kishetani na kuwa watu wa imani zaidi. Sisi tunapaswa kuepukana na matendo yote ya kishetani tuyafanyayo maishani mwetu. Leo tuyachunguze yote na kutambua ni yapi na tuoneshe utayari wa kuyaacha.
Tuwe tayari kuachana pia na baadhi ya marafiki ambao ndio chanzo cha maanguko yetu. Pale tutakapokuwa tayari kuyaacha matendo haya, ndipo na sisi tutakuwa tayari kujifungulia mlango wa neema toka kwa Mwenyezi Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni