Jumanne, Mei 04, 2021
Jumanne, Mei 4, 2021.
Juma la 5 Pasaka
Mdo 14: 19-28;
Zab 145: 10-13, 21 (K. 12);
Yn 14: 27-31.
AMANI YA KRISTO INAYO FARIJI!
Karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza ambapo tunakutana na Paulo akipigwa na mawe. Paulo anaumia sana lakini waamini wanakuja na kumzunguka huku wakimuombea na kumtia moyo na hakika anapata tena nguvu na kunyanyuka na kurudi na kuendelea na utume wake katika mji ule ule wa Listra.
Huu ni mji ambapo wao na Barnaba walipata sifa kubwa sana-wenyeji walidiriki kuwaita Miungu. Lakini leo wanatokea watu wenye chuki na kumpiga Paulo kwa mawe kiasi cha kuonekana kama amekufa. Wakristo wanapokuja ananyanyuka tena. Sisi tuwaige wakristo hawa.
Duniani wapo watu ambao kazi zao ni kuwapiga wenzao kwa mawe. Kila siku wanatafuta wa kumrushia mawe kwa maneno na chuki mbaya na kuwasema wenzao. Tusijiunge na makundi haya. Tuwatie moyo wale waliotupiwa mawe katika jamii zetu. Wapo wengi wametupiwa mawe na wanashindwa kunyanyuka. Tusiungane kuwapiga tena mawe bali tuwanyanyue hawa.
Katika somo la injili, Yesu anatuasa tutafute amani. Yesu anatuachia amani yake. Ili tuweze kuipata amani yake, lazima tutambue kwamba ulimwenguni wapo wanaochafua amani. Wapo wenye chuki ambao kazi yao ni kuona wengine waanguke tu na hufurahia kuwaona wenzao wakilia. Hivyo lazima tuepuke kushirikiana na watu wa namna hii. Tukiendelea kusikiliza maneno yao na kuruhusu siasa zao zitawale masikio yetu, hakika tutashindwa kuongea lolote lililo zuri kuhusu wenzetu na tutakuwa watu wa kutenda dhambi kila siku. Tuombe neema ya kuwa vyombo vya amani duniani. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni