Jumatano, Mei 05, 2021
Jumatano, Mei 5, 2021
Juma la 5 la Pasaka
Mdo. 15:1-6
Yn. 15 :1-8
KUONDOA MAJIVUNO NA UBINAFSI!
Karibuni sana ndugu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bwana Yesu leo katika injili, anawaeleza wanafunzi wake kwamba yeye ni Mzabibu wa kweli. Na kila anayetaka kuwa tawi katika yeye, ni lazima akubali afanyiwe "pruning". Ni lazima akubali kuachana na matendo na vilema kadhaa.
Ukweli ni kwamba hatuwezi kuja kuja kwa Yesu na kuwa tawi lake bila kuacha baadhi ya matendo yetu. Hivyo, tujitahidi kuangalia ni baadhi ya matendo yapi yanayoutuzuia kila siku na kushindwa kujiunganisha kama tawi katika shina la Bwana wetu Yesu Kristo. Wapo pia marafiki wanaotufanya tushindwe kujiunganisha vyema na shina letu yaani Yesu Kristo. Tuwe tayari kufanya maamuzi magumu. Pia tunapaswa kuendelea kujishikiza kwa mzabibu wetu yaani Yesu Kristo kwa njia ya sala. Tawi haliwezi kupata nguvu bila kujishikanisha na shina. Sisi tunapaswa kujishikanisha na shina letu, yaani Yesu Kristo kwa njia ya sala na sakramenti mabalimbali.
Tukiyaacha haya, hakika hatutaweza kuchota nguvu ya kusonga mbele. Tukiacha kusali au kuja kanisani, hakika hatutaweza kupata nguvu katika maisha yetu. Tuzidi kujishikanisha na sala.
Katika somo la kwanza, mitume wanaamua kusuluhisha mambo ya kanisa kwa njia ya majadiliano. Katika majadiliano haya, wanaheshimu viongozi wa kanisa la Yerusalemu na kwa pamoja wanatoa uamuzi utakaolisaidia kanisa. Sisi tutambue kwamba mambo yahusuyo kanisa huwagusa wengi. Kanisa sio la mtu mmoja, au kizazi kimoja tu, au zama fulani tu. Hivyo chochote kihusucho kanisa yafaa kiamuliwe kwa busara kubwa, kwa utulivu na kwa hekima bila kuweka vionjo vya mtu mmoja mmoja au kutafuta umaarufu na sifa binafsi, kuacha kuweka siasa na ubishi wa bure alimradi uonekane unajua kuongea, haya ni ya kukwepa.
Pia maamuzi yetu yafaa yawafikirie kizazi kijacho pia. Sio kwa kizazi chetu tu. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni