Jumanne. 22 Aprili. 2025

Tafakari

Jumatatu, Mei 03, 2021

Jumatatu, Mei 3, 2021
Juma la 5 la Pasaka
Sikukuu ya Mitume Filipo na Yakobo, Mitume
1 Kor 15: 1-8;
Zab 18: 2-5;
Yn 14: 6-14


TUNAITWA KUWA VYOMBO VYA HABARI NJEMA!


Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo Kanisa linaadhimisha sikukuu ya mitume Philipo na Yakobo. Mtume Philipo alihubiri huko Ugiriki na Syria wakati mtakatifu Yakobo mtume alibakia Yerusalem na alihudumu kama Askofu wa kanisa mjini Yerusalem. Mitume wote walikufa kifo shahidi.
Katika somo la injili yetu, tunakutana na mazungumzo kati ya mtume Philipo na Yesu. Cha muhimu Yesu anachomueleza Philipo ni kwamba yeye aendelee kumwamini Yesu kwani yeyote aaminiye ama kweli ataiona nguvu ya Kristo maishani mwake; Yesu anasema kwamba huyo atafanya mambo makubwa Zaidi kabisa ya yale ambayo Yesu mwenyewe aliyafanya.
Yote haya yanawezekana kwa sababu injili yetu ya leo Yesu anamwambia Philipo kwamba yeye yuko ndani ya Baba na aliyemuona yeye, amemuona na Baba pia. Hivyo Yesu anayo mamlaka makubwa kama yale ya Baba na ndio maana yote haya yanawezekana. Na ukweli wa kauli hii ya Yesu kwamba yeyote aaminiye atatenda makubwa hata zaidi ya aliyotenda Yesu ilidhihirika katika maisha ya mitume hawa. Mfano, mtume Philipo aliweza kusafiri hadi Ugiriki na Syria akihubiri injili na idadi kubwa ya watu wakimsikiliza na kumwamini na kuwezesha kuanzisha makanisa. Tukumbuke kwamba Yesu katika utume wake hakufika Ugiriki au Syria na pia idadi ya wale waliokuja kuamini maneno ya Philipo, walikuwa ni wengi zaidi ya wale walio yaamini maneno ya Yesu wakati akihubiri mwenyewe.
Kwa upande wa mtume Yakobo, yeye alikuwa Askofu wa kanisa la Yerusalem na kwa kweli idadi ya watu aliowaongoza kama wakristo nao walikuwa ni wengi zaidi ya nyakati zile za Yesu. Hapa sitaji haya yote kwa lengo la kuonesha ati mitume walikuwa wakuu kuliko Yesu bali lengo ni kuonesha kwamba mitume kwa kuwa walimwamini Yesu, waliweza kutenda makubwa hata zaidi ya Yesu-lakini tukumbuke kwamba yote haya ni Yesu alikuwa anawawezesha wao kuyatenda- yeye ndiye aliyempeleka Roho Mtakatifu na kuwezesha haya yote kuendelea kutendeka.
Katika injili yetu na kwa njia ya mifano ya hawa watakatifu wawili, twajifunza mambo makubwa: muhimu ni juu ya imani kwa Yesu. Hii ni hazina kubwa na Yesu anavyotueleza ni kana kwamba bado wengi hatujaweza kuivumbua thamani ya hazina hii. Ni kwamba matatizo yote anayokutana nayo mwanadamu, yote yanaweza kutatulika kwa njia ya imani. Magonjwa, shida mbalimbali, maumivu, umaskini, yote Mungu anayajua na kwa njia ya imani yanatatulika. Lakini shida ni kwamba wanadamu tumekosa imani. Kila siku Yesu katika mafundisho yake alihuzunika juu ya watu kukosa imani. Watu walijihangaisha na mambo mengi mno, walitumia nguvu nyingi bila mafanikio yeyote, akina Petro walivua usiku kucha wakikazana bila kasamaki chochote lakini walipokutana tu na Yesu na kufuata neno lake, waliweza kufanya makubwa na kuweza kuvua samaki wengi ajabu. Yote haya ni changamoto kwetu.
Mitume walipojaribu kuyafikiria maisha baada ya ufufuko kwa akili yao waliishia kukata tu tamaa. Lakini Yesu alipokuja kwao na kuwapatia Roho Mtakatifu-mara moja waliingiwa na nguvu kama nyati na kuanza utume bila woga kuweza kufanya mambo makubwa hata zaidi ya yale ambayo Yesu hakuyafanya wakati wa enzi yake duniani. Yote haya yatupe mwongozo na sisi. Sisi nasi tupo katika mahangaiko; magonjwa, umaskini na fujo za hapa na pale; jiulize, tuliwahi kumshirikisha Kristo kwenye yote haya? Kabla ya kwenda hospitali huwa ninasali? Nina mwamini daktari/dawa zangu bila kumtanguliza Yesu? Usikute natumia nguvu zangu tu kama wale mitume walivyokuwa wanatumia nguvu zao tu kuvua usiku kucha bila faida?
Je? Ninajiamini kwa nguvu zangu tu na nataka yote yawezekane kwa nguvu zangu? Tujichunguze.
Katika somo la kwanza tunakutana na habari kwamba Yakobo ni miongoni mwa watu ambao Yesu aliwatokea yeye mwenyewe. Tendo la mtume kutokewa na Yesu lilikuwa linamfanya mtume aongeze imani yake kwa Yesu; na mfano wa hili ni Paulo. Suala lake la yeye kukutana na Yesu lilimfanya abadilike moja kwa moja. Hata hili tendo la Yesu kukutana na Yakobo lilimbadilisha maishani na kuyaweka maisha yake yote kwa Kristo. Nasi tuige mifano ya hawa mitume. Hata sisi kwa kipindi hiki cha Pasaka, tumekutana na Kristo mfufuka. Katika Ekaristi takatifu tunakutana naye moja kwa moja. Basi tuwe na Imani atubadilishe.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni