Alhamisi, Aprili 29, 2021
Alhamisi, Aprili 29, 2021.
Juma la 4 la Pasaka
Mdo 13:13-25;
Zab 89:2-3,21-22,42:225,27 (K. 2);
Yn 13:16-20.
TUMEBAHATIKA KUWA “WATUMWA”
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Bado tunaendelea kufurahia neema na baraka tulizoletewa na sikukuu yetu ya pasaka kwa ufufuko wa Kristo na neno la Bwana leo katika injili tunakutana na Yesu akiwageukia wanafunzi wake na kuwapatia maneno ya kuwatia moyo. Maneno ya injili ya Yesu ni sehemu ya wosia wa Yesu kabla ya kifo chake. Anayatoa baada ya kuufanyia tathmini utume wake na jinsi ulivyoenenda.
Katika mwenendo wa utume wake, alikutana na vipingamizi vingi, kuna waliompokea na waliokataa utume wake. Yaani kuna waliokataa kukipokea hata kile chema Yesu alichokuwa anafanya. Ebu fikiria-katika hali yetu ya kawaida-tunatambua hali ya viwete, wakoma, bubu, viziwi, na watu wenye ulemavu mbalimbali. Mara nyingi unakuta wametengwa na unawakuta wakiwa wamevaa nguo chafu, hawajawahi kuoga, wakiwa na vidonda mbalimbali, na wakiwa wanaombaomba msaada toka kwa watu. Sasa, Yesu alijitokeza katika utume wake na kuwaponya watu kama hawa lakini cha ajabu ni kwamba walitokea watu wakamkasirikia na kumwonea wivu, wakaona kana kwamba Yesu anajipatia umaarufu sana-wakashindwa kuyaona yale mateso ya hawa viziwi au viwete.
Hivyo, wakamkejeli Yesu na kumwambia kwamba anatoa pepo au uponyaji kwa njia ya beelzebuli-yaani mkuu wa pepo. Ama kweli maneno kama haya yalikuwa ni ya kukatisha tamaa. Lakini pia katika utume wa Yesu, kuna waliompokea vizuri na kumtia moyo.
Sasa Yesu anawaeleza wanafunzi wake kwamba hata nao katika utume wao, watakumbana na hali kama hiyo, kuna watakaowapokea na wengine hawatawapokea. Na hili ni fundisho pia katika maisha yetu. Unapofanya kitu kizuri, tena kwa ajili ya watu-lazima huu ujumbe wa YESU uwe ndani ya kichwa chako pia: lazima ujue kwamba sio wote watakaokuona kwamba unafanya jambo zuri. Mwingine ataanza kukutangaza, kukusema kana kwamba unafanya kitu kibaya kama unaua mtu, watatafuta namna ya kukuibulia skendo, wataangalia jinsi uhusiano wako na wanawake/wanaume na watoto ulivyo. Watajaribu kuchunguza nyanja zote hizo lengo likiwa ni wakuangushe, usipate sifa. Mfano; wale kina mama na akina baba ambao muda wote wanapenda kutoa ushirikiano kanisani;unakuta muda wote wapo, ukitokea usafi wapo, kanisani asubuhi wapo, kwenye usafi wapo; sasa utashangaa kuona kwamba kuna watu wasiotambua mchango wao, wengine wataanza kuwatafutia kuwachafua/skendo. Sisi tusikatishwe tamaa. Tujue kwamba ni nguvu ya shetani inayofanya kazi ndani ya hawa wapinzani na lengo ni kudumaza kazi yako na utume wako mwema. Hivyo tujiandae jamani. Ukikatishwa tamaa na kuzifikiria utashindwa kufanya kitu na shetani atakuwa ndio amefaulu sasa. Lakini nyenzo muhimu ni kujiepusha na dhambi.
Jua kwamba pale unapokuwa unafanya kazi njema-hata kama ni ndani ya shirika fulani la kusaidia jamii-kuna watu ambao kazi yao ni kuchungulia tu, kuangalia je, ni makosa gani unayotenda, ni wanawake wangapi labda wanaoteswa au kutendewa maovu, ni watoto wangapi wanaoteswa. Hivyo tukibakia katika kutenda mema, hakika tutawashinda hawa wapinzani. Halafu kingine ni sisi wenyewe kutambua kwamba sio kila baya linalosemwa na watu juu ya wengine ni ukweli. Mengine ni uongo na wivu tu wenye lengo la kuwaangusha wengine. Hivyo, labda ukisikia mtu aliyekuwa anafanya kazi nzuri halafu anaibuliwa maskendo lazima kufikiria mara mbili pia. Nyingine sio za kweli.
Halafu pia tukumbuke changamoto iliyopo katika mafanikio: mtu unapokuwa unafanikiwa sana na kupongezwa kwa kazi nzuri, tutambue kwamba shetani naye huja, yeye huanza kujipenyeza na kuanza kukuletea kiburi, uvivu, uzembe na majivuno ili ile kazi yako iharibike. Hivyo, tuwe makini jamani.
Katika somo la kwanza tunakutana na mtume Paulo akiendelea na safari yake ya kwanza ya Kimisionari. Yeye mwenyewe aliuchukulia kwa umakini mkubwa ule wosia uliotolewa leo na Yesu katika injili. Alikutana na watu waliompokea lakini pia waliompiga kwa mawe na kumchapa viboko kutokana na kazi yake njema lakini yeye alisonga mbele. Mtume huyu atutie moyo hasa wale tunaofanya kazi katika ujirani na mazingira magumu, wale ambao hawaoni kitu chema toka kwetu lakini lengo lao ni kututafutia kutuchafua tu. Lakini tujue kwamba kuna watu wanaopokeaga ujumbe wetu pale tuufanyapo na kutuelewa na kumfuata Yesu. Hawa watutie moyo.
Maoni
Ingia utoe maoni