Jumatatu, Aprili 19, 2021
Aprili 19, 2021.
------------------------------------------------
JUMATATU, JUMA LA 3 LA PASAKA,
Somo 1: Mdo 6:8-15 Shemasi Stefano, akitenda ishara kubwa na miujiza kati ya watu, na kufanya watu walumbane katika Sinagogi.
Wimbo wa Katikati: Zab 119:23-24,26-27,29-30 Heri ambao maisha yao hayana hatia.
Injili: Yn 6:22-29 Yesu anaendelea na katekesi yake kuhusu Ekaristi.
------------------------------------------------
KUKUTANA NA MCHUNGAJI MWEMA ANAYETAKATISHA ROHO ZETU
Yesu anatupatia fundisho ambalo kwa paska yetu tunaweza kulitumia kama dhihirisho kwamba kweli tumefufuka na Kristo. Yesu baada ya kuwalisha watu wengi mikate na baada ya wengi kutaka kumfanya mfalme, leo wanaendelea kumtafuta; wanamtafuta wakifikiria kwamba atawapatia tena chakula. Hivyo hata lile lengo lao kutaka kumfanya mfalme ni kwamba walitaka ili labda awe akiwatengenezea chakula kwa miujuiza ili wao wale bila kufanya kazi. Yesu anatambua wanamtafuta kwa sababu ya chakula na si kwa kiu ya neno la Mungu. Naye anawaambia wazi katika lugha nzuri na ya kiupendo bila kufoka au kuchukia. Anawaambia watafute chakula cha kiroho chenye kutolewa na Yesu.
Japokuwa makutano walimtafuta Yesu kwa lengo la chakula cha kimwili, tukumbuke kwamba uwepo wao karibu na Yesu uliwapa bahati ya kufundishwa na kupatiwa chakula kifaacho. Kitendo cha kuwa karibu na maeneo matakatifu chaweza kubadili maisha yetu; mazingira yanaweza kutoa nafasi ya Yesu kuongea nasi na kubadili nia zetu na kuwa bora zaidi. Yapo maeneo au mazingira ambayo tukikaa karibu nayo-huwa vigumu kwa Bwana kuzungumza nasi. Kuhudhuria kanisani, kushika vitu vitakatifu kama rozari, au kuviweka chumbani mwetu au kwenye gari-vyaweza kutubadilisha.
Hivyo, tupende kukaa katika maeneo matakatifu. Tutambue kwamba ukipoteza uhai wako ukiwa ndani ya kanisa-wengi watakutangaza kama shahidi. Lakini ukipotezea uhai wako ndani ya vilabu vya pombe–kwa wengi utaonekana kuwa mlevi. Tupendelee kukaa katika maeneo Matakatifu ili tuweze kushindana na vishawishi vyetu. Mazingira yaweza kutufanya pia tukaanguka kwenye dhambi kirahisi. Kama unataka kutembea, pita barabara ambayo unajua itakuwa nzuri kwako itakusaidia ili uweze kutembea vizuri, maisha ya kiroho yapo hivyo hivyo, tupite barabara ambayo itatusaidia kushindana na vilema vyetu.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni