Jumamosi, Aprili 17, 2021
Jumamosi, APRILI 17, 2021,
Juma la 2 la Pasaka
Mdo 6:1-7
Zab 33:1-2,4-5,18-19,22
Yn 6:16-21
KUTULIZA DHORUBA ZETU!
Tafakari yetu ya neno la Bwana katika siku ya leo naomba tuanze kwa kuliangalia somo la injili. Katika injili hii, tunakutana na wanafunzi wa Yesu wakiwa peke yao katika bahari katikati ya dhoruba kali. Wanajitahidi kupambana na dhoruba kwa nguvu zao bila mafanikio. Ni hadi Yesu anapowafikia ndipo na dhoruba hii inapata kutulia.
Wakiwa katika dhoruba, wanafunzi walikumbwa na hofu kubwa. Matumaini yao ya kuokoka yalipotea kabisa. Hofu iliwafanya hata Yesu alipokuja wakashindwa kumtambua. Wakamuona kuwa kama msumbufu mwingine anayetaka kuwaongezea matatizo zaidi.
Yaliyowatokea mitume ndugu zangu yanazidi kututokea na sisi hadi siku ya leo ndugu zangu. Wengi wetu tumetawaliwa tayari na hofu na matatizo mbalimbali. Duniani kuna matatizo, lakini tusikubali matatizo yatutawale, na kuishinda imani yetu. Wanafunzi walipokubali matatizo yakawatawala, hakika walishindwa kusaidika, na hata Yesu anapokuja kwao, wanashindwa kumtambua kama Mwokozi; anawafanya waongezewe hofu zaidi.
Matatizo hayapaswi kutawala uhuru wetu. Wapo baadhi yetu ambao kipindi cha matatizo tunakuwa tayari kufanya kila kitu-tunafanya hata maamuzi ya kijinga. Na wapo ambao vipindi vya matatizo vimewafilisi kwa sababu ya uzembe wa kuruhusu matatizo yawatawale. Wapo ambao wameruhusu miili yao kuchanjwa, kufanya hata matendo ya aibu kwa sababu waliruhusu vipindi vya matatizo vikatawala hata uhuru wao. Hatupaswi kuwa hivi. Magumu ya maisha yatumiwe kama sehemu ya kukutana na Bwana.
Katika somo la kwanza, mitume wanaamua kurudisha utulivu katika jumuiya ya wakristo wa mwanzo kwa kuwachagua mashemasi watakaohusika na ugawaji wa mahitaji ya kila siku. Mashemasi hawa walichaguliwa ili kupambana na tatizo la kubaguliwa kwa baadhi ya wajane katika jamaa. Nyakati zetu pia tunakabiliwa na tatizo la ubaguzi-ambapo wapo wanaopewa kipaumbele au kupendelewa zaidi. Tunahitaji na sisi mashemasi watakaosaidia kuondoa ubaguzi wa namna hii. Na sisi tujitolee kuwa mashemasi wa kupambana na ubaguzi ndani ya jamii zetu. Tuondoe pia kasumba ya kuwadharau baadhi ya watu na kuwatenga. Wao nao ni binadamu. Yapaswa wapewe kipaumbele pia. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni