Jumatano, Aprili 14, 2021
Jumatano, Aprili 14,, 2021.
Juma la 3 Pasaka
Kumbukumbu ya Mt. Yosefu Mfanyakazi
Mdo 5:15-17;
Zab 34:1-8;
Yn 3:16-21.
Baba alionesha upendo mkubwa sana kwa dunia.
Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Katika somo la kwanza, wanafunzi wa Bwana wanaonja wokovu wa Bwana katika maisha yao. Bwana anamtuma malaika wake kuja kuwaokoa.
Palitokea viongozi wa Kiyahudi waliowaonea wivu na kuwafunga gerezani. Viongozi hawa waliamini sana nguvu zao wakitegemea kwamba kila watakachofanya kitafanikiwa kutokana na wingi wa mamlaka. Lakini leo Mwenyezi Mungu amewaonesha kwamba hakika ni mwenye nguvu kuliko wao. Hivyo, waache kuwatishia na kuwaonea watumishi wake. Jambo hili liliwaletea fedheha kubwa viongozi hawa. Nguvu zao zilishindwa kuwapatia sifa au kuizima kazi ya Bwana. Mungu ni nguvu ya wanyonge.
Somo hili litupatie funzo la kuacha kujiamini kupita kiasi. Twaweza kuwa na maarifa, akili, pesa, marafiki, nguvu na hata silaha. Lakini tusipomtegemea Mungu, upo wakati yote haya yataonekana kuwa bure. Zaidi sana ni kujifunza kugundua ukomo wa uwezo na mamlaka yetu na hata wa marafiki zetu. wengi wetu hatujui ukomo wao. Hizi ndizo sababu za wengi wetu kujivuna kupita kiasi.
Injili inatuagiza na kutuambia kwamba Yesu wetu alikuja ulimwenguni ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele. Baba alionesha upendo mkubwa sana kwa dunia. Sisi tutambue kwamba bado hatujajitahidi kuonesha upendo mkubwa sana kwa dunia. Bado vipo vingi ambavyo tungalipaswa kufanya ili kuisadia dunia lakini hatujafanya bado.
Muda wetu tumeutumia vibaya, wapo wagonjwa wengi na wengi wenye shida na matatizo ambao wangalipaswa ukute wamekwishasaidika kwa sababu ya mimi kutumia muda wangu zaidi na kupaaza sauti yangu zaidi. Labda tuangalie kukaa kwangu kimya kumewafanya watu wangapi wasaidike?
Hapa kwa hakika hatujajitoa bado kama inavyotakiwa. Au kama kila mmoja wetu angalikuwa anachangia kila kwaresma kwa ajili ya kanisa-je, ni watu wangapi tungalikuwa tumewasaidia. Uvivu wetu umeirudisha dunia nyuma na ndio sababu za wengi wetu kuwa maskini. Tuongeze majitoleo yetu ili wengine wasaidike. Tuache kukaa vijiweni. Tunapoteza muda mwingi sana. Ule muda wa vijiweni ungaliweza kutusaidia kufanya mengi. Wengi wetu tunaishi katika mazingira machafu, tunaumwa kila siku kwa sababu ya kukosekana kwa wenye kujitolea kuyasafisha. Tuzidishe majitoleo yetu ili dunia yetu iwe sehemu pema zaidi. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni