Jumapili. 05 Mei. 2024

Tafakari

Jumanne, Disemba 20, 2016

Jumanne, Desemba 20, 2016,
Juma la 4 la Majilio

Isa 7: 10-14;
Zab 24: 1-6;
Lk 1: 26-38


MUNGU ANAFANYA VITU VYOTE VIWEZEKANE

Leo tunapewa ushuhuda wa Imani kamili na Mama yetu Mbarikiwa. Jibu lake lilikuwa nini? “mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendwe kama ulivyo nena.”. Katika hali ya mapokeo tunaongelea hili kama “NDIO” kuu yake kwa Mungu. Kitu kimoja katika hili ni kwamba Mama yetu anajikabidhi kabisa hata kabla hajaelewa. Malaika anatoa maelezo mafupi kwake, lakini ukitazama kwa undani sio maelezo mafupi hayo yaliomfanya Mama Maria aamini. Alikuwa amesha amini, na hivyo Imani ilikuwa inatafuta uelewa. Si kwamba alisikiliza maneno haya na kuanza kuyachambua kama yanafaa au la! Alisikiliza, akayaweka moyoni na mara moja akajitoa kwa maneno yaliyo zungumzwa. Imani ya mama yetu ilikuwa ni Imani ile iliofahamu ukweli bila uelewa kamili.

Je, wewe na mimi tupo tayari kujikabidhi kwenye mapenzi ya Mungu na ukweli bila kuelewa? Je, tunamuamini Mungu zaidi kuliko tunavyo amini akili yetu ya kibinadamu? Je, tupo tayari kusonga mbele kwa Imani zaidi kuliko kuamini akili zetu pekee? Tujitahidi kuiga akili ya Imani ya Mama yetu. Aliujua ukweli kwasababu uliongelewa ndani ya moyo wake. Aliusikiliza na kujitoa na kukumbatia mapenzi ya Mungu.

“Tazama, Bikira atachukua mimba na atamzaa Mwana na jina lake utamwita Emmanueli”. Na Emanueli “Mungu pamoja nasi” hakuishi tu katika sayari yetu kwa miaka elfu mbili iliopita, bali amebaki nasi tangu daima. Kwa njia ya ubatizo Emanueli alizaliwa tena kwetu kwa maji na kwa Roho Mtakatifu. Hatuwezi kupima upendo wa Kimungu unao msukuma Mungu wa milele kuingia katika mioyo yetu midogo. Jibu letu linapaswa liwe kama la Maria. Tunapaswa tujifungue wenyewe katika undani wa Kristo, tumruhusu Kristo abadili mahusiano yetu mabaya, na kazi zetu mbaya.

Sala: Bwana, natamani kukuamini wewe kwa akili yangu yote, moyo wangu wote na nguvu zangu zote. Nisaidie niweze kukusikia wewe ukiongea niweze kujibu kwa Imani kamili na ukarimu. Bwana naomba niige Imani kamili ya Mama yako kwa kusali daima naye, ‘naiwe kwangu kama ulivyo nena”. Mama Maria, utuombee. Yesu, nakuamini wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni