Alhamisi, Aprili 15, 2021
Alhamisi, Aprili 15, 2021
Juma la 2 la Pasaka
Mdo 5:27-33
Zab 33: 2, 9, 17-20
Yn 3:31-36
KUJAA NEEMAA: NI KUISHI KATIKA KILE MUNGU ALICHOKUPA!
Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Tafakari yetu ya neno la Bwana leo, katika somo la kwanza, Mtume Petro anakiri hadharani kwamba hawawezi kuacha kumheshimu Mungu na kumheshimu mwanadamu. Viongozi wa Kiyahudi walikuwa wametoa amri kwamba waache kuhubiri kwa kutumia jina la Yesu. Mitume wanakataa kufuata amri ya viongozi hawa kwa sababu walikuwa wamepokea amri kutoka kwa mtawala mkuu zaidi-Yesu Kristo. Amri hii ilikuwa takatifu, hivyo walishindwa kuacha kuitii.
Kwa nguvu ya Kristo, waliweza kushukiwa na Roho na pia kufanya miujiza mbalimbli na kuweza kujipatia furaha kubwa zaidi. Namna hii ilikuwa sio rahisi kwa wao kuacha kuitii amri ya Mwenyezi Mungu na kufuata ya mwanadamu.
Mitume hawa wanapaswa kutufundisha jambo muhimu. Wengi wetu tunawatii wanadamu kuliko Mungu. Tupo tunaowaogopa wanadamu, tunahofia kufukuzwa kazi au kuachwa bila kuolewa na baadhi wamekuwa tayari hata kubadili dini kwa sababu ya hofu katika maisha yake. Tunaogopeshwa na wanadamu wenzetu. Yafaa tujifunze kuona ukuu wa Mungu wetu ndani ya maisha yetu.
Kila mmoja leo anapaswa kuchunguza kile kinachomtia hofu, kinachomfanya asilale-je, kinatoka wapi? Ni cha Mungu? Vitu vya namna hii hutufanya tushindwe kumtii Mwenyezi Mungu. Tunatumia muda mwingi kuviwaza. Havipaswi kutusumbua kiasi hiki. Lazima tujue kwamba Mungu ana uwezo kuliko mambo haya. Mungu anapaswa kutawala akili zetu.
Kwenye somo la injili, Yohane anatuhimiza kumwamini Yesu. Anatueleza kwamba Baba amempatia mamlaka makubwa juu yake. Hivyo anapaswa kuabudiwa. Asiyemwamini hakika atapotea. Mitume katika somo la kwanza wametuonesha mfano wa kumwamini.
Yesu alikabiliwa na upinzani, wapo waliopinga asiabudiwe. Mitume wanaonesha kwa msisitizo kwamba anapaswa kuabudiwa. Sisi tuzidi kujikabidhi mikononi mwa Yesu wetu. Kila mmoja aongeze bidii yake ya kumwamini Yesu popote pale alipo. Tuwe watu wa kuongeza bidii tupate kumwabudu Yesu kwa utakatifu zaidi.
Maoni
Ingia utoe maoni