Alhamisi, Aprili 08, 2021
Alhamisi, Aprili 8, 2021.
Oktava ya Pasaka
Mdo 3:11-26
Zab 8:2,5-9
Lk 24:35-48
UFUFUKO: KUONDOA HOFU NA KUKUMBATIA FURAHA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Bado tunaendelea kufurahia neema zilizoletwa na pasaka na leo tunamkuta Yesu akiwatokea wanafunzi wote wakiwa ndani ya chumba na anaomba kipande cha samaki na kukila mbele yao. Kitendo cha kufanya hivyo hakikuwa na maana ya kuonesha kwamba mwili wa Yesu uliofufuka ulihitaji kula na kunywa tena. Lengo lake lilikuwa ni kuwaonesha kwamba yeye si mzimu kama wale watu waaminivyo kwamba mtu aliyekufa huwa anazunguka zunguka kwenye yale maeneo waliyoishi nao watu. Lengo lake lilikuwa ni kuonesha kwamba yeye ni yule aliyekufa akafufuka na kweli mwili wake umefufuka na ndio maana ameweza hata kula kwani ingekuwa ni miili ile ya mizimu hakika isingeweza kula. Hivyo alitaka ale mbele yao kuwahakikishia kwamba hakika ni yeye kafufuka. Habari za namna hii zilizidi kuwaletea mitume ahueni na baadaye ziliwaimarisha kiimani na kuona kwamba hakika Kristo wao ana nguvu.
Jambo hili linaonekana katika somo la kwanza ambapo Petro kwa nguvu ya jina la Yesu ameweza kumponya kiwete na anatumia tukio hili kuwatangazia waamini wote kwamba ni kwa nguvu ya Yesu, yule waliyemuua na sasa kafufuka, ndiye huyu ambaye kwa nguvu zake mtu huyu kaweza kuponywa. Hivyo, anataka wote waliohusika katika kumtukana na kumkana Yesu waongoke na wamrudie Yesu kwa kuungama dhambi zao zote na kumrudia huyu Yesu ili wapate uzima.
Ndugu zangu, sisi nasi tunapaswa kumpeleka huyu Kristo mfufuka kwa wengine. Kuna watu ambao ni wagonjwa miaka na miaka, hawawezi kuamka hapo walipo. Nasi tupeleke habari za matumaini za Kristo mfufuka kwao ndugu zangu. Kuna watu ambao wamenuniana miaka na miaka, kuna watu ambao wakikutana hawaangaliani machoni-wote hawa tunapaswa kuwapelekea habari za Kristo mfufuka kwao. Wengine ni maskini, hawajawahi kuvaa hata nguo kama yako, wao wanaziona na kumezea mate tu, wengine wanakuona na simu yako na kumeza mate tu, hawajawahi kushika kitu kama hicho, akina mama wengine hata nywele zao hazijawahi kuonja shampoo au mafuta au hata kukalikitiwa, wote hao ni watu wetu na raia wetu. Peleka habari ya furaha kwao Pasaka hii. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni