Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Aprili 05, 2021

Jumatatu, Aprili 5, 2021.
Oktava ya Pasaka
Mdo 2:14,22-32
Zab 16:1-2,5-11
Mt 28:8-15.
KUMWABUDU BWANA MFUFUKA!

Ndugu zangu wapendwa, bado tunaendelea na octava yetu ya pasaka na sasa tupo katika jumatatu ya pasaka. Kipindi cha pasaka tunafurahia jinsi Kristo alivyotuletea uhuru, jinsi alivyoyafanyia mataifa mambo makubwa naya ajabu. Hili ndilo tunalojikumbushia. Juzi tulisikia kwamba usiku ule wa Kristo kufufuka katika wafu kwa kweli ulikuwa ni nuru, nuru inayowaangazia wanadamu wote, nuru inayotuletea furaha, kutuondoa katika shimo la shetani.
Lakini katika injili ya leo, hii nuru ilikuwa imekataliwa, ikauawa na Wayahudi kwa kumsulibisha kama mtakatifu Petro anavyosema katika somo la kwanza. Lakini Yesu alivumilia hayo yote na akawa amewasamehe maovu yao yote waliyomtendea. Sasa, alitegemea kwamba atakapofufuka, wao wenyewe wangegundua kosa lao ili watubu na wamkubali kwamba Yesu ni Masiha, waje kwake, wafufuke naye na kuwa wafuasi wake kama akina Petro walivyotubu. Lakini cha ajabu wao wanamkataa Yesu tena, wako tayari kulipa pesa ili waendelee kumzima Yesu. Sasa, tujiulize, huyu mtu wa namna hii hata Mungu ikiwa atamwadhibu kutakuwa na shida yoyote? Embu niambie, wewe umeshampiga, akakaa kimya, umeshamuua akakusamehe, sasa kafufuka unataka tena kuendelea kupambana naye-ebu fikiri. Kwa kweli walikuwa wanazima nuru ya Kristo mfufuka.
Hii ni tabia ya kiburi na majivuno; hawa walikuwa hawakubali kuabika. Hivyo wakataka wafiche ukweli ili waonekane ni wema bila kujua kwmaba wanazima mwanga wa Pasaka. Hata sisi tupo wa namna hiyo ndugu zangu. Kuna wakati unakuta mwenzako anakuzidi, na kapata zaidi kuliko wewe, au “point” aliyoiongea ni nzuri. Lakini wewe kwa kufikiri labda atajipatia ujiko sana, unaamua kuizima point yake ili asije akakuzidi lakini baadaye wewe unakwenda kuitumia hiyo point yake hiyo hiyo. Jamani, tuache tabia kama hizi. Hapa tunazima nuru ya Kristo mfufuka.
Kingine, somo hili linatoa onyo kali kwa wale wanaomiliki vyombo vya habari kama magazeti na pia waandishi wa habari. Nyie mnao usemi mkubwa katika jamii kwani mnaweza kuwafikia wengi. Sasa, lakini ni habari gani unazotoa? Ni uongo au kupendelea? Jamani, hakikisheni habari za ukweli ndizo zipaswazo kuwafikia watu, tuache habari za kupotosha. Wengine ni wale wanaotumia mitandao, usiposti habari za uchochezi au za uongo, au za kupotosha maadili. Kwa mfano, mimi naandikaga “ASALI MUBASHARA” na hivyo nia group langu la watu wengi. Nikiandika asali ya kupotosha mafundisho nitawapotosha wengi na hapa nitakuwa nazima nuru ya kristo mfufuka. Hivyo, lazima niutumie mtandao vizuri si kwa kupotosha. Tusizime mwanga wa Yesu mfufuka.

Wengine, ni wale wenye pesa-sasa wewe pesa yako unaitumiaga vipi? Unatumia katika kuzimia haki au kutetea haki? Mfano, kama pesa yako inatumika kununulia watu pombe hadi walewe washindwe kuwa watu na wachukiwe na familia zao, au wewe unatumia kuwasuport vizibiti mimba au kutoa mimba, angalieni haloo. Au hata vyombo vyako kama unatumia kutangazia kondomu-unazima habari ya hii nuru ya Kristo iletwayo paska hii. Unataka kuwaambia watu watende dhambi zaidi.
Hivyo, tuhakikishe kwamba kila tulichonacho hakizimi ile nuru iliyoletwa na Kristo mfufuka-namna hii tutafanikiwa, wale wote wanaoshindana na nuru hii, kama kazi yako ni kuizima nuru hii kweli hutafika popote, utalima, utaruka, utajinyoosha: lakini utajikuta hufiki popote. Hivyo, tuiache nuru ya Kristo ikiwa katika kuwaka siku zote zote na tufanye kazi zinazofanya nuru hivyo iendelee kuwaka. Mfano, kuja jumuiya, kuja kanisani, kujiunga na mashirika mbalimbali, kuposti picha zenye maadili safi ya kanisa, kutumia mtandao katika kuendeleza kazi ya Bwana. Tuache kuutumia kwenye kusambaza habari za uzushi au uchochezi. Tuangalie haya. Tusipotoshe ukweli.

Maoni


Ingia utoe maoni