Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Machi 22, 2021

Marchi 22,2021
JUMATATU, JUMA LA 5 LA KWARESIMA

SOMO 1 Dan.13:41-62
INJILI Yn. 8:12-20
Twende kwa Yesu tupate Mwanga.
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika Zaburi yetu ya wimbo wa katikati tunakutana na ujumbe-Bwana ndiye mchungaji mwema sintapungukiwa na kitu. Haya ni maneno ya Zaburi ya 23. Mzaburi anashuhudia tumaini lake kwa Mungu kama mchungaji. Wanyama kama kondoo ni wanyama dhaifu mbele ya wanyama kama simba na chui. Bila uwepo wa mchungaji mahiri, wanyama kama hawa huraruliwa kwa haraka mbele ya simba.
Bila mchungaji mahiri, wanyama kama hawa hawataweza kula majani;-watanyanyaswa tu. Ni tofauti na wanyama jeuri kama simba au chui na fisi.
Katika somo la kwanza, tunagundua kwamba kati ya wanadamu, wapo ambao ni kama kondoo na wengine ni wajeuri. Kondoo hawana nguvu au mabavu kama Susana anavyoonekana katika somo la kwanza. Wale wazee wanaomhukumu Suzana tunawafananisha na wanyama kama Simba. Hawa wanakuja kwa lengo la kurarua kila wakati. Hawa huwainulia wengine mabaya, huwaonea watu, hutumia nguvu zao kuwafaidi kondoo.
Katkai ulimwengu tutakutana na watu kama hawa. Yesu alikutana na viongozi wa Kiyahudi waliompeleka kama kondoo asiyekuwa na hatia, wakampiga bila huruma. Sisi tunapaswa kumweka Mungu kuwa kinga yetu. ulimwenguni tutakumbana na watu kama hawa. Wapo baadhi yetu ambao kuishi nao au kufanya nao kazi ni kugumu zaidi kuliko kukutana na simba.
Tumtegemee Mungu. Tunapaswa kumwita Mungu kila wakati. Katika kipindi chetu cha kwaresima, ni kipindi cha kumuita Mwenyezi Mungu. Atuepushe na maadui wetu. Wapo wanaotutakia mabaya. Lakini kwa nguvu ya Mungu tutawashinda. Mungu atatuinulia watu kama akina Danieli ambao watakuja na kututetea.
Yesu anasema katika injili ya leo kwamba yeye ni Nuru ya ulimwengu. Na yeyote amfuataye, hatakuwa akitembea gizani bali atakuwa na uzima wa milele. Twende kwa Yesu tupate Mwanga. Wengi wetu katika ulimwengu, bado tunaishi katika giza, bado tunafuata mikumbo ya wadhambi, kama umati wa leo katika somo la kwanza uliotaka kumteketeza Suzana.
Danieli alipata mwanga toka kwa Mungu. Itakuwaje kama sisi sote tutaomba na kupata Mwanga toka kwa Yesu ili tuweze kutoa hukumu zenye kufaa? Wengi katika jamii wamepakwa matope kutokana na ukosefu wa watu kama kina Daniel. Wengi wamepoteza kazi zao au kushindwa kesi au hata kupoteza maisha kutokana na kufuata wasemacho umati/mob. Tuwe makini kuchambua kile kiamuliwacho na umati. Bwana Yesu atupe Mwanga wa kufanya maamuzi ya namna hii.

Maoni


Ingia utoe maoni