Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Machi 12, 2021

Ijumaa, Machi 12, 2021,
Juma la 3 la Kwaresima

Hos 14:2-10;
Zab 81:6-11,14,17;
Mk 12:28-34

CHAGUA KUMPENDA MUNGU!

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Naomba tuanze kwa kuliangalia somo la kwanza: hapa nabii Isaya anawaeleza wana wa Yuda juu ya faida za kumrudia Bwana. Anamueleza kwamba hakika atapata faida kubwa sana. Muda wake hautapotea tena ovyo, nguvu na rasilimali zake hazitapotea tena bure, wataachana na kuishi katika hofu, watakuwa na amani na kulima kitu na kuingia ndani ya tumbo lake na kufurahi.
Israeli ilipoteza muda na rasilimali zake kwa sababu ya kukosa kumshirikisha Bwana katika shughuli zao.
Sisi tunaalikwa leo tumrudie Bwana, hakika tutapata maendeleo ya kiroho na hata kiuchumi. Ukweli ni kwamba dhambi hutufanya tupoteze rasilimali zetu vibaya, fedha nyingi zinatumika katika kutekeleza dhambi, uasherati na ulevi hutumia fedha zetu vibaya, fedha ambazo zingaliweza kutumika katika kutuendeleza. Pia dhambi hutufanya tutumie muda wetu vibaya-uasherati hutufanya tutumie muda wetu ambao ungaliweza kutumika kutupatia maendeleo zaidi. Hata uangaliaji wa picha mbaya katika mtandao hutufanya tutumie muda vibaya. Wanafunzi wengi mashuleni wanafeli mitihani kutokana na dhambi-utumiaji mbaya wa muda wetu. Sisi tunaalikwa kama Yuda leo, Isaya anatuita tumrudie Bwana na hakika tutaipata faida zaidi.
Katika injili yetu, Bwana Yesu anamueleza Mwandishi kwamba hayupo mbali na ufalme wa mbinguni kwa tendo lake la kupenda jibu lililotolewa na Bwana. Kila mmoja wetu leo hayupo mbali na ufalme wa mbinguni. Bidii kidogo tu inatuwezesha kufika kusogea na kumfikia Bwana-kimkiri Yesu kuwa Bwana na mfalme. Sisi tuzidishe bidii na hakika tutamsogelea Bwana kwa ukaribu zaidi na kupewa ufalme wake.
Kila mmoja popote alipo tuongeze bidii, tumkiri Yesu kama Bwana na mfalme wetu na hakika tutaingia kwake mbinguni na kupokelewa naye na kuurithi ufalme wake.

Maoni


Ingia utoe maoni