Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Februari 27, 2021

Jumamosi, Februari 27, 2021,
Juma la 1 la Kwaresima

Kumb 26: 16-19;
Zab 119: 1-2, 4-5, 7-8;
Mt 5: 43-48

KUTAMANI KUWA MKAMILIFU

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana tutaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati hapa tunakutana na zaburi inayosema kwamba heri walio kamili katika njia za Bwana; heri wale waishikao sheria ya Bwana kwani Bwana atawabariki daima na kuwa mfano kwa wengine; watu wakiwaona watatiwa matumaini. Haya ni maneno ya mzaburi wetu. Maneno haya yanaambatana vyema na maneno ya ujumbe wa neno la Bwana katika somo la kwanza ambapo Musa anawaambia wana wa Israleli wawe waaminifu kwa zile sheria za Mungu walizomwahidia kuzishika. Kwa kuzishika sheria hizi, Mwenyezi Mungu anaahidi kuwabariki na kuwafanya kuwa taifa kubwa sana. Nao watalifanya jina lake liheshimiwe pote na watu wote watakuja kwa Mungu wa Israeli kumwabudu na hivyo Mungu wa Israeli atapata sifa. Hii ndiyo faida ya kuzishika amiri za Mungu.

Ndugu yangu, jua kwamba unapoishika amri ya Mungu, unamfanya Mungu asifike, apate sifa na utukufu. Mfano, kitendo cha mashahidi kufa kwa ajili ya Yesu, kilimfanya Yesu atukuke, apate utukufu. Hivyo, ndugu zangu, tujitahidi leo. Tuzishike amri za Mungu, tukizishika tunawafanya wenzetu wamsifu na kumtukuza Mungu. Unapokataa kuzishika amri unawakwaza wenzako na Mungu atatukanwa kila kukicha ndugu zangu. Siku hizi Yesu anadharauliwa na baadhi ya watu Fulani kwa sababu tumeshindwa kuonyesha mfano mzuri na watu kuishia kumdharau Yesu.

Injili yetu inatuambia kwamba lazima sisi kama Wakristo maisha yetu yaonyeshe utofauti. Nisi ishi kwa kuongozwa na mitazamo ya watu wa dunia. Wanadamu wengi tunafuata siasa ya jino kwa jino, ninakulipa kile ninachopokea kutoka kwako. Ninakuwa rafiki kwa yule ninayejua kwamba naye ni rafiki, namsaidia yule nijuaye kwamba atakuja kunisaidia baadaye. Yesu anapinga hili na kusema kwamba tunapofanya hivi ni kinyume cha wito wetu, hufanyi cha ziada kwani hata wenye dhambi hujifanyia hivi hivi-hivyo tukifanya hivi hatutakuwa tofauti na wenye dhambi. Sisi tunategemewa kufanya Zaidi-na anayeshika dini anategemewa afanye Zaidi. Mfano, kosa moja laweza kufanywa na watu wawli tofauti-lakini unashangaa watu wanauliza limefanywa na nani. Unapokutwa limefanywa na mkristo au mtu wa dini, basi malalamiko yanakuwa makubwa Zaidi. Hivyo, tujue kwamba tunategemewa kutenda Zaidi kama watu wa dini. Fundisho hili litupe nguvu na moyo wa kuwasaidia maskini na wenye shida tunaokutana nao kila siku. Hawa hawawezi kutulipa na kama hatutaelewa fundisho hili la Yesu, kamwe hatutaweza kuwasaidia. Wakituomba mchango hatutawapa. Lakini kama tutaelewa fundisho la Yesu, basi tutakuwa radhi kuwaasaidia muda wote. Fundisho hili litutie moyo katika kujitolea Zaidi kwa ajili ya maskini. Tumsifu yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni