Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Februari 21, 2021

Februari 21, 2021.

------------------------------------------------

JUMAPILI, DOMINIKA YA 1 YA KWARESIMA

Somo la 1: Mwa 9:8-15 Baada ya kumuokoa Noah na familia yake kutoka katika gharika, Mungu anaanzisha upya Agano lake-makubaliano kati yake na watu. Upinde wa mvua ni kiashirio cha ukumbusho wa Agano hilo.

Wimbo wa katikati Zab: 24:4-9 “Njia zako Bwana ni kamilifu na unawapenda wanaoshika Agano lako”.

Somo la 2: 1 Pet 3:18-22 Mt. Petro anasema maji ya wakati wa Noah ni ishara ya maji ambayo kwasasa tunaokolewa nayo kwa njia ya Ubatizo.

Injili: Mt 1:12-15 Baada ya kubatizwa na Yohane Mbatizaji, Yesu alikaa siku arobaini jangwani. Akiwa huko alijaribiwa na shetani. Marko anatoa kwa ufupi juu ya kujaribiwa kwa Yesu na mwanzo wa kuhubiri kwake.
------------------------------------------------

TUMEOSHWA TUKATAKATA NA MAJI!

Katika somo la kwanza linatuambia kwamba Mungu hakatishwi tamaa na sura ya uovu. Anaingilia ili kujenga tena upya na kufanya mapya. Anajenga ubinadamu mpya na kuahidi baraka na vitu vizuri: “ninaanzisha agano jipya na ninyi, na kila mnyama na ninyi…maisha hayata haribiwa tena kwa njia ya gharika” (Mwa 9:9-11). Huu ni ujumbe wa matuamiani na faraja kwamba Mungu hasubiri watu wawe wazuri ndio awe mkarimu kwao. Mungu anawabadilisha waweze kuwa viumbe wapya.

Katika somo la pili Petro naye anachukuwa habari ya maji ya gharika ya kipindi cha Noah na kuelezea habari za ubatizo. Noah aliokolewa na safina ambayo Mungu alimuagiza aitengeneze na yeye na familia yake pamoja na wanyama waliokolewa, hivyo uumbaji, uhuru kutoka katika dhambi, uweze kuanza tena. Maji ya ubatizo vile vile huharibu na kuangamiza hali ya zamani na kumfanya mtu kuwa mpya, na kuonesha kuwa mwisho wa dhambi, huondoa uharibifu wa mwanadamu na kuunda maisha mapya na kutia Roho mpya.

Katika somo la Injili Yesu amekaa jangwani akifunga kwa muda wa siku arobaini, na huko anajaribiwa na shetani. Yesu alikutana na watu mbali mbali katika safari ya maisha yake. Alikutana na viongozi wengi katika ulimwengu huu: wenye madaraka, wanauchumi na viongozi wa dini (Masadukayo, ma Sanhedrin, na Makuhani wakuu) hata kukutana viongozi wa dini ya Kiyahudi waliomhubiri Mungu kuwa mkali sana na adui wa wadhambi (Mafarisayo): malaika waliomhudumia, tunaweza kusema ni wazazi wake, watu waliomsaidia katika utume wake, wale wote walioshiriki katika maisha yake na kuyafuata yale aliowaambia-waliomtumikia-walioshirikiana naye katika kazi ya wokovu. Lugha ya Biblia na picha ina maana maisha yote ya Yesu yalikuwa ni kupigana kati yake na yule mshawishi. Hali ambayo inatupata sisi wote tunamfuata pia. Daima tupo katika mapambano kati ya wema na uovu, na muovu anajaribu kutuvuta kwake daima ili tuache njia iliyo nzuri.

Vishawishi vipo. Ni matokeo ya maanguko ya wanadamu wa kwanza. Yanatoka katika udhaifu wetu lakini pia kutoka katika yule muovu. Yesu hakukubali kuanguka katika vishawishi alivyokuwa jangwani na wala hakuanguka katika kishawishi katika maisha yake yote. Aliyashinda na kuteseka kwa ajili ya hayo. Hili linatuambia kwamba anaweza kuwa kiongozi wetu na mfano wetu wa kuiga wakati tukiwa katikati ya vishawishi kila mara na kila siku. Wakati mwingine tunaweza kujisikia wa pweke tuliotengwa katika jangwa la dhambi zetu. Tunaweza kujisikia kama vile mnyama mkali wa tamaa zetu unatushinda. Tunaweza kujisikia yule muovu anatunyemelea. Sawa, Yesu alipatwa na haya pia. Aliruhusu kupitia haya kwa kushiriki ubinadamu wetu. Kwa njia hii ni Yesu anayeweza kukutana nasi katika jangwa letu. Yupo tayari anatusubiri, akitutafuta, akituita sisi. Ni huyu aliyeshinda vishawishi vya muovu jangwani, ndiye atakaye tuongoza kuepuka. Kwahiyo, kama jangwa lako ni mahangaiko ya maisha sasa, au ni majaribu mbali mbali, Yesu anataka kukutana nawe akuongoze katika njia iliyo njema. Alimshinda yule wa jangwani na jinsi alivyokuwa, hivyo anauwezo wakushinda jangwa lolote lile katika maisha yako.

Kwaresima ni kipindi cha kuamua kujinasua katika dhambi. Yesu anasema katika Injili ya leo kwamba “huu ndio wakati mtimilifu. Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Injili”. Kama tunataka ubatizo wetu ulete maana na kutusaidia nilazima tuyaweke maneno ya Yesu katika maisha yetu. Jipatanishe na mwingine ambaye mmekosana naye. Jitahidi katika sala ya ndani na kujiunga na Mungu. Fanya madadiliko sahihi na anza vita kati yako na dhambi, hasa ile dhambi ambayo unayo irudia kila wakati ambayo huwezi kujinasua. Amua kutoka moyoni pambana nayo na hakikisha unaachana nayo. Kuwa tayari kusimama kwa tunu za Kristo hata pale ambapo kuna vishawishi vingi katika maisha.

Epuka sehemu mabazo wewe mwenyewe ukikaa unajua kabisa zinakupeleka kwenye dhambi. Kwepa marafiki wabaya wanaokupeleka kwenye dhambi daima. Wale ambao kwa hakika unatambua kabisa nikikaa nao daima hawanipeleki kwenye utakatifu wananipeleka kwenye dhambi tu. Hata kama ni ofisini ambapo wenzako wanafanya madili ya pesa ambazo sio halali, kuwa tayari kuwa tofauti nao na onesha kweli Imani yako inaambatana na matendo yako. Hata kama watakutenga na kukuona mbaya, hakika haupo mwenyewe upo na Yesu. Epuka vishawishi vyovyote vile. Ashindaye mpaka mwisho kama Yesu alivyoshinda daima hupokea taji. Tumuombe Mungu atusimamie.

Sala:
Bwana, ninakubali upendo wako mkamilifu kwangu. Nina amini kwamba unanipenda mimi kiasi kwamba nitaweza kuvumilia mateso, kuelewa mateso yote. Ninakuomba nikutane nawe katika jangwa la maisha yangu. Ninakuomba nikuruhusu wewe uniongoza katika sehemu tulivu na yenye maji. Yesu nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni