Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Februari 19, 2021

Ijumaa, Februari 19, 2021,
Ijumaa baada ya Jumatano ya majivu


Isa 58: 1-9;
Zab 51: 3-6, 18-19;
Mk 9: 14-15.

NJAA KWA AJILI YA MUNGU!



Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza, Mungu kupitia kinywa cha nabii Isaya anatangaza kwamba kufunga ni tendo takatifu na lenye matunda makubwa kwa mwanadamu. Na Popote pale ambapo Mwanadamu alimlia Mungu kwa kufunga na kutenda matendo ya kufadhili na hakika hakuachwa. Wana wa Israeli walielewa faida zilizopo katika kufunga lakini walitumia mfumo mbaya na hivyo kufunga hakukuwaletea faida au neema maishani.
Leo anawaeleza kwamba kufunga kwao lazima kuendane na matendo mema, mageuzi ya Roho ili aliyeko pembeni asaidike. Kama tunafunga halafu tunabakia kuwa wachoyo, hakuna mgonjwa yoyote anayefaidika toka kwangu, au maskini aliyeko karibu nami hapati nafuu, hakika kufunga kwangu hakuna faida. Kufunga lazima kuendane na kuthibiti matendo na vilema vyetu, lazima yaendane na kuthibiti midomo yetu, kuthibiti kitakachoonwa na macho yetu, au kusikiwa na masikio yetu. Kauli za vinywa vyetu zinapaswa kuwa safi na kumtia moyo msikilizaji. Lazima pia tupambane na chuki na shari ndani ya moyo wetu.
Huu ndio mfungo utakaotuletea neema na hakika tutaweza kuona mabadiliko. Wengi wetu hatuyaoni mabadiliko maishani mwetu yaletwayo na mfungo kwa sababu ya matendo mabaya. Kipindi cha kufunga hakiendani na kudhibiti kauli zetu. namna hii ni kupoteza muda.
Kwenye injili, Yesu anawaeleza wanafunzi wa Yohane mbatizaji katika injili kwamba wanafunzi wake hawawezi kufunga kwa sasa kwani wako bado na Bwana arusi. Yesu ndiye Bwana arusi na wanafunzi wa Yesu walipokuwa na Yesu, walipaswa kukitumia kipindi hiki kuchota toka kwa Yesu, kujifunza mafundisho yake wayaelewe na watakapokuwa wenyewe baada ya Yesu kuondoka kwao. Wakiwa na Yesu, Yesu alikuwa mtatuzi wao wa kila kitu, lakini atakapokuwa ameondoka, hakika itabidi wao wenyewe wapambane kwa kufunga ili wapate utatuzi wa mambo. Hapa ndipo itakapowabidi kuungana na Yesu kwa njia ya kufunga na sala ili waweze kuyatatua.
Sisi ndio wakati wa kufunga kwani yapo mengi tunayopaswa kuungana na Yesu kwa njia ya kufunga ili tuyatatue. Sisi tusiache kufunga. Kufunga kunakufanya usafiri na Mungu. Akina Musa, Daudi na Ester walifunga wakiomba na Mungu aliwasikiliza.

Maoni


Ingia utoe maoni