Alhamisi, Februari 18, 2021
Alhamisi, Febrauri 18, 2021,
Alhamisi baada ya Jumatano ya majivu
Kum 30: 15-20;
Za 1: 1-4, 6;
Lk 9: 22-25
KUIPATA ROHO KWA KUPOTEZA ULIMWENGU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuingalia injili yetu ambapo tunakutana na Yesu akiwaeleza wanafunzi wake juu ya mateso ambayo yeye kama Masiha angeyapokea huko Yerusalem. Habari hizi hizi zilikuja kwao kwa mshtuko mkubwa na walizipokea kwa huzuni. Hii ni kwa sababu zilikuwa kinyume cha matarajio yao; wengi kati yao walikuwa hawategemei kitu kama Masiha wao angeingia katika mateso makali hivi. Hii iliwashtusha kwa sababu nao walitambua kwamba Bwana wao akipata mateso basi na wao watayapata, itawabidi nao wabebe msalaba uliobebwa na Bwana wao. Hivyo, waliona kwamba walikuwa wanakwenda kuishia maisha ya shida. Lakini Yesu alizidi kuchukuliana nao hivyo hivyo taratibu na kuwaongoza taratibu hadi walipokwisha kutambua nini umuhimu wa msalaba na cha kushangaza ni kwamba baada ya Yesu kuwapa Roho Mtakatifu, walikuja kuona kwamba mateso ni kitu kidogo tu. Hivyo walikuwa tayari kuteseka, kuchapwa viboko, kufungwa na hata kufa kifo dini. Lakini ukiambiwa walikoanzia, kulikuwa mbali.
Ndivyo na sisi ndugu zangu, pengine wengine tumeingia maisha ya ndoa au ya utawa tukiwa na malengo tofauti. Tulifikiri kwamba baadhi yetu tumefaidi, tungekuwa na raha, hakutakuwa na mateso na labda leo nina misukosuko, ninakabiliana na umaskini, ndoa inasumbua, mume au mke hanisikilizi, utawa hauendi, mambo ni magumu kila wakati, sijisikii ile raha. Injili yetu ya leo inatuambia kwamba mitume nao walikutana na hali kama hii. Walijiona kupotea-lakini walipopokea Roho Mtakatifu, walijiona kwamba wapo mahali sahihi na hawakutaka watoke pale walipokuwapo bali walikuwa tayari kupata kifo dini pale.
Katika somo la kwanza, Musa anawaambia wana wa Israeli wachague kati ya kifo au uzima. Na anawaeleza kwamba endapo watachagua njia ya kifo, hakika atawaangamiza, na anaapa kabisa kwamba atawaangamiza. Njia ya kifo siku zote inakuwaga rahisi rahisi, inakataa mateso. Lakini inaongoza motoni. Sisi tunaonyeshwa na Yesu leo kwamba kuubeba msalaba, kupitia ile njia aliyopitia mkombozi wetu, ndio njia iongozayo kwenye uzima ambako tunakusikia katika somo la kwanza.
Masomo yetu haya ni onyo kwetu hasa kwa wale walioishia kuwakimbia wake au waume zao kutokana na umaskini au ugonjwa. Nawambia hapa mmechagua njia ya kifo. Wale mliotelekeza watoto wenu walipopata magonjwa au binti apatapo mimba wewe unamkana au hata kama umewahi kumkana mtu yeyote ili ujiepushie na aibu. Hapa tulidumbukia katika kuchagua njia ya kifo, njia rahisi. Ni wakati wa kuomba msamaha kwa Mungu leo.
Shukrani za pekee ziwafikie nyie mliosafiri na wake au waume zenu katika ugonjwa au umaskini bila kuwatelekeza, wale mliokubali kubeba misalaba ya wenzenu, mlioachiwa watoto na mabinti zenu mkalea bila kuwatelekeza au kutupa. Shukrani sana. Hapa mlichagua njia ya uzima. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni