Jumanne, Februari 16, 2021
Jumanne, Februari 16 2021
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa
Mwa 6: 5-8; 7: 1-5, 10;
Zab 29: 1-4, 9-10;
Mk 8: 14-21.
CHACHU ULIMWENGUNI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana, tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati: hapa tunakutana na maneno yasemayo Bwana atawabariki watu wake kwa amani. Yeyote aliye na Bwana anabarikiwa kwa amani.
Anayebarikiwa leo katika masomo yetu ni Nuhu. Yeye basi alionekana kuwa mwema kati ya wanadamu wote wa ulimwengu, hivyo anapokea baraka, anatunzwa na Mungu, anaamriwa atengeneze safina itakayomkinga na maangamizi ya gharika. Nuhu hakufuata mkumbo wa ulimwengu, hakuamua kwenda na wakati na kufikiri jinsi ulimwengu ulivyofikiri. Hili lilimuokoa.
Sisi ndugu zangu tujifunze kusoma alama za nyakati, tuachane na kasumba ya kuiga kila kinachotendwa na ulimwengu. Ulimwengu haupaswi kutuongoza, sisi tuuongoze. Sisi wakristo tunapaswa kuwa Nuhu wa vipindi vyetu. Hivyo itatubidi tuondoe kasumba ya kutaka kunusa nusa kila kitu kitokacho ulimwenguni. Sio kila kitu kilichopo ulimwenguni tujaribu kushiriki, si lazima niingie kila bar au kila aina ya kumbi za starehe. Sio lazima ati ni nunue kila toleo jipya la simu au kwenda tamasha la kila mwanamuziki. Dunia inahitaji Nuhu wa kutufundisha namna hii.
Ili tuwe Nuhu yafaaa tuondokane na tamaa. Tudhibiti vionjo vyetu kila mara.
Kwenye somo la injili, Yesu anawaambia wanafunzi wake wajiepushe na chachu ya Mafarisayo. Hawa walikosa imani kwa Yesu, walimuonea Yesu wivu na kutaka asiheshimiwe na yeyote. Walikuwa na chuki naye na utayari wa kumfanyia chochote kiovu. Kwa kitendo chao cha kuanza kuona hofu kwa kutokuchukua mikate, yamaanisha kwamba bado walikosa imani, walishindwa bado kuutambua ukuu wa nguvu yake.
Sisi tuishi kiimani, tuwakubali wenzetu katika jamii waliojaliwa vipaji kuliko sisi. Tumtumainie Mungu, tuombe abariki na yote tuyafanyayo. Atuepushe na chachu ya ukosefu wa imani, tuishi tuwe imani siku zote, Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni