Ijumaa, Februari 12, 2021
Ijumaa, Februari 12, 2021,
Juma la 5 la mwaka wa Kanisa
Mwa 3: 1-8;
Zab 32: 1-7;
Mk 7: 31-37.
EPHATHA, FUNGUKA!
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo linatueleza kwamba wana heri wale waliosamehewa kosa lao, wasiokuwa na hatia tena, ambao dhambi zao zimeondolewa. Ambao hawahesabiwi kosa tena na Mungu.
Zaburi hii inatumika kutilia mkazo kile kisemwacho katika somo la kwanza. Hapa tunakutana na wazee wetu wakitenda kosa, kosa la kukosa utii, wanakiuka amri ya Mwenyezi Mungu, wanakuwa na kiburi, wanatafuta madaraka ya kutaka kufanana na Mungu mwenyewe. Wanataka kujikomboa toka katika mamlaka ya Mwenyezi Mungu. Hili ni kosa kubwa, kutaka kutwaa madaraka ya Mwenyezi Mungu, kutaka kumpindua Mungu na kumkosesha madaraka. Mungu aonekane kama sisi, awe mmoja wetu. Ndilo kosa linalotendeka leo. Mungu atawapa adhabu kali. Lakini basi zaburi yetu inatuambia kwamba tufurahi kwani hili kosa lilikwishasamehewa kwa Yesu aliyekufa msalabani.
Hivyo tuna neema tele, hatuishi tena chini ya laana, tupo na Yesu, tumesamewa kosa. Shukrani kwa Yesu Kristo. Kwa njia yake tunakila sababu ya kucheka; hakuna haja ya kilio tena. Tumshukuru Yesu, Yesu ametufundisha kwamba ni lazima kunyenyekea mbele ya Mungu. Sisi tubakie katika kunyenyekea.
Katika somo la injili, tunakutana na Yesu akimponya mtu aliyekuwa bubu na kiziwi na huyu anapona na watu wanafurahi kabisa. Yesu ni sababu yetu sisi kufurahi. Leo amemtembelea huyu bubu na kiziwi na hakika amepata kusema na kusikia. Sisi tuombe na Yesu atutembelee leo maishani kama anavyomtembelea huyu mgonjwa wa leo. Tusikubali Yesu apite pembeni yetu na kutuacha, bila kufanya chochote.
Tumguse Yesu leo, tumlilie, aje kwetu na atuguse. Hakika tutafaidi kama huyu bubu na kiziwi anavyofaidi leo. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni