Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Februari 11, 2021

Alhamisi, Februari 11, 2021,
Juma la 5 la Mwaka wa Kanisa

Mwa 2: 18-25;
Zab 128: 1-5;
Mk 7: 24-30.

KUDHIHIRISHA IMANI!

Ndugu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo katika wimbo wetu wa katikati tunakutana na Zaburi isemayo: heri kila mtu amchaye Bwana, hakika huyu amebarikiwa. Huyu atakuwa na uzao uliobarikiwa, na hakika atabarikiwa zaidi na Bwana. Kumcha Mungu ndio chanzo cha Mwanadamu kubarikiwa.
Tunaona kwamba zaburi hii inatumika leo kusisitizia kile kinachoelezwa katika somo la kwanza ambapo tunakutana na mwanadamu anaumbwa katika hali ya unyenyekevu, hana hata nguo ya kuvaa-lakini wanadamu hawa wangejibariki kwa kumcha Bwana, kumcha Bwana ndiko kutakakowawezesha kukabiliana na kila aina ya changamoto. Kumcha Bwana ndiyo iliyopaswa kuwa rasilimali yao kuu. Tunatambua katika Biblia kwamba pale walipokataa kumcha Bwana, hakika walianguka vibaya. Sisi tusiache kumcha Bwana, tutambue kwamba tumeumbwa ili tumche Bwana, huu ndio wajibu wetu wa kwanza. Hivyo lazima kumcha Bwana kila siku.
Tuibariki siku yetu kila siku. Tukikataa kumcha Bwana, ndipo tutakapoanguka. Wengi tupo katika maisha ya duni kwa sababu ya kukataa kumcha Mwenyezi Mungu.
Katika somo la injili, Yesu anamjibu kwa ukali mama ya kutoka Tiro na Sidoni. Jibu hili halijajaa ukatili kama tukilichunguza vizuri-Yesu alitaka kuitambua imani yake, hii ni kwa sababu mama huyu alikua amezoea imani ya mazingaumbwe, maajabu yaliyofanywa na baadhi ya wanamazingaumbwe katika nchi yake ya Kiyunani. Hivyo kuna hatari kwamba angaliishia kumuona Yesu kama miongoni mwa wanamazingaumbwe, na ndio sababu za Yesu kumjibu kwa ukali namna hii ili kumpatia ujumbe kwamba miujiza yake ipokelewe kiimani na si waichukulie kama mazingaumbwe.
Mama huyu alikuwa na imani, na jibu lake laonesha unyenyekevu, na pia alielewa kwamba miujiza ya Yesu ni kwa ajili ya watu wenye imani na si kwa ajili ya wale wanaomuona Yesu kuwa kama wanamazingaumbwe.
Sisi tuwe watu wa imani ndugu zangu. tutambue kwamba huwezi kutendewa muujiza na Yesu kama huna imani, sisi tuwe watu wa imani. Tusije mbele ya Yesu tukiwa katika hali ya kutokujiandaa, lazima tujiandae kila siku. Tumuache Yesu atende mwenyewe

Maoni


Ingia utoe maoni