Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Februari 09, 2021

Jumanne, Februari 9, 2021,
Juma la 5 la Mwaka wa Kanisa

Mwa 1:20 - 2:4;
Zab 8: 4-9;
Mk 7: 1-13.

KENGELE YA KANISA!

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo zaburi yetu ya wimbo wa katikati ni zaburi ya 8 “jinsi lilivyotukufu jina lako ulimwenguni kote Ee Bwana.” Hii ni zaburi ya Daudi inayotukuza uumbaji. Inashangilia jinsi uumbaji unavyomtangaza Mwenyezi Mungu. Pia inatambua jinsi mwanadamu alivyopewa hadhi na Mwenyezi Mungu, hadhi ya kutawala na kuvihudumia viumbe vingine. Pia inatambua thamani ya kila kiumbe-hata kachanga “wasifika na vinywa vya watoto wadogo na wanyonyao.” Kila kiumbe kina hadhi pekee mbele ya Mungu.
Zaburi hii inatumika kutilia mkazo ujumbe wa uumbaji katika somo la kwanza. Leo tunasikia juu ya uumbaji wa mwanadamu na jinsi anavyokabidhiwa kuvitunza viumbe vingine. Tunakabidhiwa jukumu la kuutunza ulimwengu wote. Tukiwa ulimwenguni sisi ni mawakili wa Mungu. Hivyo tutambue wajibu wetu, tuwe watu wa kuvipenda viumbe, tusifurahie vikiteseka. Sisi tutambue kwamba ni wamawakili wa Mungu hapa ulimwenguni.
Katika somo la injili, Yesu anawaambia Wafarisayo kwamba ni lazima waanguke miguuni mwa Mungu ili wapate kufundishwa sheria za Mungu. Ukosefu wa unyenyekevu wa namna hii uliwafanya washindwe kuzitambua sheria za Mungu, wakaishia kutunga zao ambazo haziwezi kuwapatia wokovu.
Sisi tutambue kwamba ni viumbe vya Bwana. Ni lazima tuwe watu wa kuanguka miguuni pa Mwenyezi Mungu kuomba msaada wa nguvu zake, tumwambie Bwana nioneshe sheria zako, ili kwa njia ya hizi tuweze kupata wokovu.
Huu ndio unyenyekevu unaohitajika mbele ya Mungu. Sisi ni viumbe vyake, tuwe na utayari wa kuanguka miguuni mwake. Tusipokuwa watu wa kuanguka miguuni pake, hakika tutakuwa tunatwanga maji katika kinu. Ndicho walichofanya mafarisayo. Hawakumuomba Mungu awafundishe sheria zake. Wakawa wanajitahidi kila siku kufanya kazi ya Bwana lakini wakashindwa tu.

Maoni


Ingia utoe maoni