Alhamisi, Disemba 15, 2016
Alhamisi, Desemba 15, 2016,
Juma la 3 la Majilio
Isa 54: 1-10;
Zab 30: 2-13;
Lk 7: 24-30
UNA MWALIKO WA UFALME WA MUNGU!
Ni nani aliye mkuu katika Ufalme wa Mbinguni? Yesu anamsifia Yohane kuwa mkuu kati ya uzawa wa wanawake! Lakini katika hali hiyo hiyo Yesu anasema aliye mdogo katika Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohane! Hii inaonekana kama vile inachanganya kama tusipo elewa Yesu alitaka kukamilisha nini kwa ajili yetu! Yohane ni wa mwisho na mkuu kati ya manabii wa Agano la kale. Alikamilisha kazi zote muhimu za manabii-kumuonesha Yesu, Mwana-kondoo wa Mungu na Masiha. Yohane alimuonesha Yesu katika mto Yordani “tazama Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia” (Yn 1:29). Yohane aliona kwa mbali kile Yesu ambacho atakikamilisha kwa kifo chake pale Msalabani-ukombozi wetu kutoka katika bonde la dhambi na mauti na kutufanya wana wa Mungu na raia wa Mbinguni.
Kama Yohane, sisi pia tunaitwa tutoe ushahidi wa maisha ya mwanga na ukweli kama Yesu Kristo. Sisi tunaitwa kuwa wafuasi wa Yesu. Tunaitwa kuitikia wito kwa kukubali mafundisho na ukombozi uliotolewa na Yesu ili tupokee mwaliko wa ufalme wa Mbinguni. Tunaweza kupatwa na kishawishi cha kujiona wema kama wale viongozi wa dini kipindi cha Yesu na kukosa mwaliko wa Yesu. Usikatae mwaliko wake, bali upokee kwa moyo wote. Katika kuupokea kwa moyo wote, utashangaa Mungu atakubariki hata katika hali ambayo huwezi kuelezea.
Sala:
Bwana, nisaidie niweze kuingia katika mwaliko wako kila siku katika maisha yangu. Ninaomba kila wakati nichague mapenzi yako matakatifu na niyaishi bila kujibakiza. Yesu, nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni