Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Februari 03, 2021

Jumatano, Februari 3, 2021,
Juma la 4 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 12: 4-7;
Zab 103;
Mk 6: 1-6.

MAMBO YA KAWAIDA YANATUFANYA TUWE TAYARI KUPOKEA YASIO YA KAWAIDA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati, mwimbaji wa zaburi hii anatueleza kwamba upendo wa Bwana ni wa milele kwa wale wanaomcha. Zaburi hii inatueleza kwamba Bwana anapendezwa na wale wanaomcha, wanaompatia heshima ya pekee. Kumheshimu Mungu hutufungulia mlango wa Baraka.
Somo la kwanza linatueleza kwamba Bwana humletea magumu na mateso yule anayempenda-lengo la mateso haya ni kutufundisha ili mpendwa wake apate kuchukua tahadhari na kujifunza na kupata maarifa zaidi ya kuyafahamu maisha. Hivyo, mwandishi wa kitabu cha Waraka kwa Waebrania anatutia moyo kwamba tusonge mbele, tupige moyo konde na kujitia moyo pale tukutanapo na mateso.
Hapa mwandishi anataka kutufundisha juu ya thamani kubwa iliyoko katika mateso. Kila mateso lipo fundisho toka kwa Mwenyezi Mungu atakalo kutufundisha. Pia ipo faida atakayotupatia zaidi. Sisi tuombe kutambua na kuiona faida iliyopo katika mateso.
Wengi tunashindwa kuivuna neema inayopatikana ndani yake. Ndani yake kuna fundisho kubwa. Tusikubali teso lolote litupate bila kuona ujumbe Mungu anaotaka kukuambia kupitia teso hilo.
Kwenye somo la injili, watu wa nyumbani mwake Yesu wanapata nafasi ya kuhubiriwa vizuri na Yesu. Yesu anafafanua neno vizuri. Lakini badala ya kumpokea ili awe mwalimu wao na kumfaidi zaidi, wao wanamkataa kwa sababu anatokea familia ya chini na wa palepale kijijini. Hivyo wanamkataa. Hivyo Yesu anakwenda kuwafaidisha watu wa mataifa mengine na wao wanabaki bila kitu.
Sisi tujifunze kuacha dharau. Dharau zimetufanya tushindwe kuiendeleza jamii. Wengi wenye uwezo wameachwa na cha ajabu wanaochaguliwa ni wale wasio na uwezo yote kwa sababu ya dharau. Mambo haya huirudisha jamii nyuma. Wanaoachwa wangekuwa msaada zaidi kwa jamii. Tujifunze unyoofu nakupokea ujumbe wa kinabii ili tuweze kuwa wema zaidi.

Maoni


Ingia utoe maoni