Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Januari 31, 2021

Jumapili, Januari 31, 2021,
Juma la 4 la Mwaka wa Kanisa


Kum 18:15-20
1 Kor 7: 32-35
Lk 1: 69-75;
Mkc1: 21-28


Watu tunaishi katika mazingira mbali mbali na hivi kutofautiana kimaisha. Wengine wagonjwa, wengine wazima, dhaifu, maskini na fukara. Hata hivyo, ubatizo unatuunganisha, wote tunakuwa kitu kimoja. Yaani, kila mmoja wetu amepewa nafasi ya pekee ya kueneza Injili kadiri ya hali yake.
Kum 18:15-20
Nabii anaonesha mamlaka yake, pale anapoutangaza ujumbe wa Mungu, kwa watu kiaminifu, na maneno yake yanabeba ujumbe wa Mungu. Kama nabii, akianza kuhubiri ujumbe au mawazo yake binafsi, huo unakuwa si unabii, bali anakuwa hana tofauti na mtu yeyote anayeongea mambo ya kawaida.
Katika Agano la Kale alikuwa Musa na manabii wengine. Katika Agano Jipya walikuwa mitume ambao baada ya kumpokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste walitangaza Habari Njema kwa bidii yote. Sasa kazi hiyo hufanywa na jumuiya yote ya wakristo. Sisi sote ni manabii kwa kuisikiliza sauti ye Mungu na kuisambaza popote ulimwenguni. Kwa kuwa tu manabii hasa kwa njia ya ubatizo wetu, tunapaswa kuangalia hali halisi ya watu, familia na taifa ndipo tulete mwanga wa Habari Njema kwao.
Katika injili ya leo tunajifunza kuwa, Yesu anafundisha kama mtu mwenye mamlaka ya pekee. Ni tofauti kabisa na Waandishi ambao walitoa mafundisho yasiyo yao. Wao walinukuu mafundisho ya watu wao. Lakini Yesu alifundisha kwa njia tofauti. Yeye alitumia mamlaka yake mwenyewe. Alizungumza kwa uhuru wote. Alizungumza kadiri ya sauti ya Mungu ilivyomwongoza.
Watu waliokuwa tayari kumsikiliza Yesu walipata faraja sana, kwani maneno yake yaligusa mioyo yao. Ndiyo kusema, ujumbe wenye mamlaka toka kwa mtu mwenyewe, una nguvu ya pekee ya kuvuta watu waweze kumsikiliza.
Yesu aliwapa watu ujumbe wa Mungu. Ujumbe huo ulikuwa ni maisha yake yeye mwenyewe. Watu walionja kuwa Yesu alizungumza kile alichoamini na kuona kuwa ni cha kweli. Alifundisha kile ambacho yeye mwenyewe alikiishi.
Najiuliza mwenyewe, Je, ninapozungumzia habari za Mungu, au za kanisa, kweli ninayaamini hayo nisemayo? Tumesikia kuwa, baada ya Yesu kutoa mafundisho, mtu mwenye pepo mchafu alitokea ndani ya sinagogi.
Nyakati zile za yesu, haukuwepo utaalam wa kisayansi kuhusu madawa, bakteria, kifafa au ugonjwa wa akili. Yeyote aliyepatwa na matatizo ya kiafya yanayohusiana na akili, alidhaniwa kuwa ana pepo wachafu. Kadiri ya imani ya Wayahudi waliamini kuwa pepo wachafu walitoka baharini, angani, na kwenye makaburi. Hakuna aliyekuwa na uhakika kamili kwamba wapi hao pepo wachafu walitoka.
Mtu mwenye pepo mchafu ni yule anayepingana na utakatifu wa Mungu. Pepo huyo humtesa binadamu na humzuia asiwe katika ubinadamu wake halisi. Mtu anayeteswa na pepo mbaya anakuwa kama mtu aliyetengwa. yuko uhamishoni, anakosa amani na hana furaha.
Vilevile, aliyepagawa na pepo mchafu, anakuwa bado hajakutana na Kristo. Anakuwa na nguvu za giza kama vile za ubaguzi wa rangi, ukabila, imani za ushirikina, ulevi, ubinafsi n.k.
Kulikuwa na mapambano makali kati ya Yesu na huyo aliyepagawa na pepo, kwani mtu mwenye tabia za hapo juu hapendi kuacha tabia zake hizo chafu.
Yesu amekuja kumkomboa mwanada mu kutoka katika nguvu zile zina zomfanya asiwe huru, aonekane amete ngwa na yuko uhamishoni. Kama wakristo tunapaswa kutambua kuwa tuko vitani pamoja na Kristo. Mkristu aliyejiweka mikononi mwa Yesu Kristo, ataushinda uovu, na kumshinda mwovu. Anapaswa atambue ni uovu gani anaopambana nao kila siku ambao humfanya ajione hayuko huru, au uovu unao wafanya wengine wasiwe huru, la mateka.
Tuwe wakweli mahali ambapo pamejaa uovu. Tena, tuyaishi yale ambayo tunayahubiri kwa watu iii wao watuone kuwa kweli sisi ni wakristo.
Tukutanapo na mtu asiyelijua Neno a Mungu kutokana na jinsi anavyoishi, tumwelimishe, tusikubali kushindwa eti kwa sababu ya woga kwa kuwa moyo wake umekuwa mgumu, bali tuwe wavumilivu mpaka hapo atakapopata mwanga wa Kristo.
Tunaalikwa leo pia kuwaombea kwa namna ya pekee wale ambao wanafanya kazi ya kulitangaza Neno Ia Mungu, hasa makatekista, mapadri, maaskofu na watawa.

Maoni


Ingia utoe maoni