Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Januari 18, 2021

Jumatatu, Januari 18, 2021.
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 5: 1-10;
Zab 110: 1-4;
Mk 2: 18-22.


MAISHA YASIO UNGWA, MAISHA MAPYA

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza Mwandishi anajitahidi kufafanua juu ya upekee wa nafasi ya kuhani mkuu. Anasema kwamba ni mtu maalumu, yeye hutwaliwa na Mungu kati ya wanadamu ili aweze kuwaombea wanadamu. Mwandishi anasisitiza kwamba ni vyema kuhani mkuu atwaliwe kati ya wanadamu ili aweze kuwasaidia vyema kwani ataweza kufahamu shida zao na kuweza kuwa mwombezi na muunganishi wao mwema pamoja na Bwana.

Hii ni tabia mojawapo kuu ya kuhani mkuu. Yesu anafaa sana katika hili kuwa kuhani mkuu kwa sababu yeye alichukua hali ya ubinadamu na hivyo anajua vyema hali ya mwanadamu na hivyo anaweza vyema kuwakilisha udhaifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu. Ukuhani wa Yesu unacho cha pekee zaidi. Yesu sio tu mwanadamu bali pia ni Mungu. Hii imempatia upekee wa kuweza kusimama mbele ya Mungu na kutuombea.

Hivyo ndugu zangu, Yesu ndiye kuhani wetu mkuu. Yeye ni Mwombezi wetu. Tumkimbilie, yeye ni mpatanishi wetu mwema na Baba. Nasi tujitahidi kuwa wapatanishi kama Yesu. Tusiendelee kuruhusu magomvi na chuki zitawale ndani ya jumuiya zetu. Kila mmoja wetu avae roho ya kikuhani ya kiupatanishi.

Yesu katika injili ya leo anajionesha kwamba yeye kweli ni mtetezi mwema hasa pale anapojibu hoja za Mafarisayo juu ya kufunga. Yesu anawatetea vyema wanafunzi wake. Kweli ni kuhani Mkuu. Ni mtetezi wetu sote. Hivyo kila mmoja wetu ajitahidi kumpokea Yesu. Yesu anapaswa kupokelewa katika viriba vipya, katika moyo mpya na si moyo wa zamani. Lazima tuiandae mioyo yetu kwa ajili ya upya unaoletwa na huyu kuhani.

Wengi wetu tumeshindwa kumfaidi Yesu kwa sababu tunakwenda kwake na viriba vya zamani, mioyo ya zamani. Hatutaki kubadilika kwanza kabla ya kumfuata. Tujitahidi kubadilika.

Maoni


Ingia utoe maoni