Jumatano, Januari 20, 2021
Jumatano, Januari 20, 2021,
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa
Wiki ya kuombea umoja wa Wakrsito (Januari 18-25, 2017)
Ebr 7: 1-3, 15-17;
Zab 110: 1-4;
Mk 3: 1-6
DHAMBI INATIA MAWINGU MAISHA YETU!
Ndugu zangu karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linatueleza juu ya ukuhani wa Yesu. Inasisitizwa kwamba ni mkuu kuliko ule wa Kiaroni, ule wa wana wa Israel. Wa kwake ni wa kimilele, Melkizedeck anaelezwa kama mkuu na mtu wa haki.
Kitendo cha Abrahamu kumpatia zawadi, tena moja ya kumi ya mali kilimaanisha ukuu aliokuwa nao huyu Melkizedek. Hii ni kwa sababu mara nyingi aliyedhaifu ndiye anayepaswa kumpatia kodi aliye mkuu. Abrahamu ni baba wa taifa la Israeli yote. Sasa, kama Abrahamu alikuwa tayari kukubali kumwinamia na kumpatia Melkizedek kuhani fungu la kumi la mali yake, yamaanisha ukuu wa Melkizedek, kwamba yeye alikuwa mkuu kuliko Abrahamu, baba wa taifa la Israeli na hata hivyo hata ukuhani wowote wa wana wa Israeli utakuwa ni chini kuliko wa huyu Melkizedeck kwa sababu kama Mzee wao mwenyewe alikubali kumwinamia, basi taifa la Israeli yabidi limwinamie na kumsujudu.
Yesu ndiye Melkizedeck wetu na kuhani wetu. Kama kuhani, anabakia milele akituunganisha na Baba. Twende kwa Yesu, tupeleke shida zetu kwake, tusimame mbele yake, tumweleze mahitaji yetu yote. Yeye ni mpatanishi wetu mwema.
Abrahamu aliweza kupata baraka toka kwa Melkizedeck kwa sababu alikubali kutoa hata sehemu yake ya kumi kuanzisha urafiki. Sisi tutumie rasilimali, akili na muda wetu kuanzisha urafiki na Yesu na si katika ulevi au urafiki mbaya.
Somo la injili tunakutana na Yesu akiendelea kuzozana na Wafarisayo juu ya Sabato. Anaambiwa kwamba haitii Sabato kwa kufanya tendo jema. Yeye anawaeleza kwamba Sabato msingi wake mkuu upo katika kuwatumikia wenzetu. Nasi tutambue hilo. Tutambue kwamba unapoanza kumtumikia mwenzako, kuna kauvivu na kunyanyapaa kunakoanzaga kutokea. Sisi tujiandae kupambana na haka kauvivu ndugu zangu ili sabato zetu ziwe katika kumtumikia Mungu zaidi.
Maoni
Ingia utoe maoni