Alhamisi, Januari 21, 2021
Alhamisi, Januari 21, 2021,
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa
Ebr 7:25 – 8:6;
Zab 40: 7-10;
Mk 3: 7-12
KATIKA SAFARI YA KUKUTANA NA YESU!
Tazama nimekuja ee Bwana ili nipate kuyafanya mapenzi yako. Haya ni maneno ya utayari na unyenyekevu tunayokutana nayo katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati leo.
Nabii Isaya alitoa jibu la namna hii alipokuwa anajiandaa kuchukua kazi ya Bwana. Naye Samweli vilevile alishauriwa kutoa jibu la namna hii mbele ya Bwana ili apate kuipokea na kuitimiza kazi ya Bwana.
Lakini siku ya leo zaburi hii inatumika kuelezea utayari aliokuwa nao Bwana Yesu katika kujitoa na kuipokea kazi ya Bwana na kuwa kama kuhani na kama mkombozi na mwombezi wa wanadamu. Kwa utii na utayari wake aliweza kuutendea ulimwengu mengi; utii wake uliweza kumpendezesha Mungu kuliko sadaka nyingine yoyote.
Nasi ndugu zangu tutambue kwamba utii wetu kwa Mungu utatuwezesha kuutendea ulimwengu mengi zaidi kuliko mali zetu au nguvu zetu. Viongozi wa taifa la Israeli kama Sauli walishindwa kulitendea taifa mengi kutokana na ukosefu wa utii. Makuhani wengi wa taifa la Israeli pia walishindwa kuuletea ulimwengu baraka kwa sababu ya ukosefu wa utii pia. Wao hawakuishi miiko yao ya kikuhani na hili liliwafanya wasiweze kuuletea ulimwengu faida. Sisi tuwe na utii.
Tukumbuke kwamba hata kwa upande wa Musa-pale alipokosa utii aliishia kuadhibiwa na kushindwa kuuingia na kundi lake kwenye nchi ya ahadi. Tutambue thamani ya utii.
Yesu katika injili anajidhihirisha kuwa kuhani mkuu. Anawaalika wote kuja kwake na kuwapatia uponyaji. Sisi ndugu zangu yatupasa kujifunza kwenda kwa Yesu na kumpelekea mahitaji yetu na nia zetu. Bado tumeshindwa kumtumia Yesu vizuri na ndio maana tunaishi bado katika wasiwasi mkubwa na tamaa nyingi bila mpangilio. Twende kwa Yesu.
Tusiwe kama haya mapepo ya kwenye injili-wanakiri Yesu kuwa ni mwana wa Mungu lakini hayamtumainii wala kufuata mwongozo wake. Sisi tumkiri na kufuata muongozo wake kwetu maishani-tuache kuwa kama haya mapepo.
Maoni
Ingia utoe maoni