Jumapili, Januari 24, 2021
Jumapili, Januari 24, 2021,
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa
Yona-3:1- 5,10
1 Kor 7:29-31
Mk 1: 14-20
“Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu”. Leo BY anatualika tuwe wavuvi wa watu. Kwa maneno mengine, masomo ya leo, yanatukumbusha kuhusu wito wetu, ambao ni wito wa Mungu kwa kila mmoja wetu. Wito unapaswa kuitikwa, na mwiitikio huu kubadilika na kuwa majitoleo. Kama watu tuliokomaa kiakili tunapaswa kuwa wa kweli ktk majadiliano, ktk kutafuta ushauri, na kumuomba Mwenyezi Mungu.
Hebu, nijaribu kuanika matukio mbalimbali ya kweli, yaliowatokea watu mbalimbali ktk kuutambua wito wao. Tukio la kwanza, ni ktk maisha ya Mt. Antoni, Abati. Mara baada ya kifo cha wazazi wake, aliachwa yeye mwenyewe pamoja na dada yake mdogo. Na alikuwa na miaka kumi na mitano tu. Mara baada ya miezi sita ya kifo cha wazazi wake, siku moja alienda kanisani kama ilivyokuwa kawaida yake. Mara alianza kufikiri juu ya maisha ya mitume, jinsi walivyoacha kila kitu, na kuamua kumfuata BY. Na jinsi watu mbalimbali ktk Matendo ya Mitume walivyouza kila kitu na kuleta walivyovipata mikononi wa mitume. Akiwa na mawazo haya kichwani aliingia ndani ya kanisa. Ilitokea kuwa siku hiyo, Injili iliyosomwa, ilikuwa inamuhusu mtu tajiri. “Kama ukitaka kuwa mkamilifu ukauze ulivyonavyo na uwagawie maskini, hivyo ndivyo utakavyojiwekea hazina mbinguni, na kisha njoo unifuate”. Antoni alijisikia kuwa hili linamuhusu yeye na ni wito wake. Hivyo alienda nyumbani na kufanya mipango ya kugawanya mali zote, ili zisiwe kizuizi kwake ktk kumfuata BY. Na alibakiza mali kidogo kwa ajili ya dada yake, mali nyingine aliwapa maskini na wahitaji. Kwa mara nyingine tena alipokuwa kanisani alisikia sauti ya BY ikimwambia ktk injili “usiisumbukie kesho”. Hakuweza kusubiri zaidi ya hapo, alitoka nje na kwenda kugawa hata zile mali alizoziweka kwa ajili ya dada yake, na kumuweka dada yake chini ya uangalizi wa wanawake waaminifu, ili waweze wamlee. Naye aliamua kumfuata By ktk maisha ya upweke.
Tukio jingine ni la maisha ya padri mmoja, yeye alikuwa kifungua mimba ktk familia yao. Kadiri alivyokuwa anakuwa alifanya maamuzi ya kuwa padri. Muda ulipomdia, aliwasiliana na mkurugenzi wa miito, na mkurugenzi huyo alikuja kuonana na wazazi wake. Mkurugenzi alimuuliza baba wa kijana, yakuwa mtoto wake ni kifungua mimba ktk familia, na mara nyingi tunafahamu kwamba kifungua mimba ndiye anayekabidhiwa majukumu ya kuitunza familia, na sasa huyu anapenda kuwa padri, je mpo tayari kumruhusu kufuata maisha haya? Mnajua baba alijibu nini? Ndiyo ninafahamu kabisa. Lakini kama kesho huyu mwanangu wa kwanza akifariki ni nani atakayeangalia familia yangu? Kwa hiyo sina kizuzi kabisa. Kwa hiyo alijiunga na maisha ya upadre na kuwa mwangalizi wa familia kubwa zaidi ya Mungu.
Mfano wa tatu, unamuhusu mtu mwingine, ambaye hakuweza kuwa padre. Huyu kijana alitamani sana kuwa padre, lakini mama yake alimkatalia katukatu. Mama yake aliendelea kumwambia kila siku, muda wako bado wewe endelea na masomo kwanza. Hivyo aliufuata ushauri wa mama yake na kuamua kuendelea na masomo. Hatimaye alikuwa mwanasharia, tena mwanasharia mzuri tu. Lakini alikosa furaha maishani kwa sababu matumainio yake yalikuwa mengine. Ili kujisahaulisha haya, alianza kunywa pombe. Mwishowe alioa, lakini siyo kwa mapenzi yake bali kwa kulazimishwa na mama yake. Hata hivyo hakuyafurahia maisha hayo ya ndoa. Kutokana na hilo, kulikuwa na migogoro mingi kati yake na mke wake. Hivyo aliamua kuongeza unywaji wa pombe, na kurudi nyumbani usiku wa manane. Hatimaye alianza kushindwa kutimiza majukumu yake kama mwanasheria, na hivyo kupoteza ajira yake. Alifanana na kichwa. Mara nyingine alikuwa anashituka usingizini na kuanza kukimbia uchi mitaani. Siku moja alivyokuwa anakimbia uchi barabarani huku alikuwa usingizini, alipatwa na ajali mbaya iliyomuondoa duniani.
Kwa hiyo tunasikia mifano yote mitatu, jinsi Mungu alivyowaita watu mabalimabali na jinsi walivyowajibika. Mwenyezi Mungu anamwita kila mmoja wetu ktk kuendeleza kazi zake hapa ulimwenguni. Ktk somo la kwanza tumeona miito miwili. Wito wa kwanza ni wa Yona ambaye anatumwa kwenda kuhubiri, lakini anajaribu kuukimbia wito huu. Wito wa pili ni kwa waninawi, hawa wanaitwa kutubu, nao wanaitika wito huu na kuwajibika ipasavyo. Ktk somo la pili Mt. Paulo anawaambia Wakorintho, kuwa wito wao ni wa pande mbili, yaani kwa maisha ya hapa duniani na kwa maisha ya baadaye. Thamani ya mwanadamu, mali walizo nazo, na hata ndoa, vinahusiana na thamani ya uzima ujao na ambao hamna mwisho.Na ktk injili tumesikia juu ya wito wa Petro. Andrea, Yakobo na Yohane. Wanaacha kila kitu na kumfuata BY ili waweze kufuata nyayo zake na kuendeleza kazi zake.
Sisi nasi tunafanya nini? Je tumeridhika na maisha na mambo madogo madogo tunayoyafanya ktk maisha yetu ya kikristu? Je tunaridhika na maisha yetu ya kawaida ya kila siku ktk kujaza matumbo yetu na kujaribu kuwa na mali?au tunapenda kutafuta kitu zaidi na kujikusanyia hazina ktk ulimwengu ujao? Je nini ni ulio wito wetu wa kikristu? Je tumejaribu kutafakari wakati wo wote?
Maoni
Ingia utoe maoni