Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Januari 28, 2021

Alhamisi Januari 28, 2021.
JUMA LA 3 LA MWAKA


Ebr 10: 19-25;
Zab 24: 1-6;
Mk 4: 21-25
------------------------------------------------

MWANGA WENU UANGAZE

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Zaburi yetu ya wimbo wa katikati leo inatueleza habari za yule atakayepanda mlima mtakatifu wa Mungu. Huyu ni yule aliye na mikono safi na moyo mweupe, asiyeamini miungu ya uongo au kumsengenya jirani yake.

Ndugu zangu, kiukweli, ulimwenguni kuweza kukutana na mtu kama huyu ni vigumu sana kwani ulimwenguni huishi wanadamu na si malaika. Lakini somo la kwanza linatupatia matumaini makubwa juu ya hili-kwamba Yesu ndiye mwenye kutuwezesha kuupanda huu mlima mtakatifu. Yesu ni kuhani mkuu, yeye ndiye mwenye kutupatanisha na Baba, tunaweza kupaingia patakatifu kwa DAMU YA YESU.

Yesu ndiye mwenye kutupatia ujaasiri wa kupaingia patakatifu. Hivyo tuthamini ukuu wa damu hii, ndiyo inayotuokoa.Tukifunikwa na damu hii, hakika hakuna kitakachotusumbua, tunapata ujasiri wa kupaingia patakatifu. Leo tuombe kufunikwa na damu hii. Usipite bila kumwambia Mungu hili kwamba nifunike kwa damu yako nipate kupaingia patakatifu. Sentensi moja tu yaweza kuokoa maisha yako na maoteo yote ya yule mwovu.

Katika injili, Yesu anatumia mfano kwamba taa lazima iwekwe juu ya kiwango ili ipate kuwaangazia wengine. Sisi kwa ubatizo wetu ni taa ya ulimwengu-na huwa tunajitahidi kujiweka juu ya kiwango ili tutoe mwanga. Lakini shida ni kwamba hatutoi mwanga wowote na ndio maana hatujulikani kwamba tupo. Hii ni kwa sababu taa isiyotoa mwanga sio rahisi kuonekana. Inahitaji itoe mwanga ili yenyewe ipate kuonekana na kuwaangazia wengine.

Sisi tutambue kwamba tunangaa kutokana na matendo mema na Sala. Hapa ndio tunapata kutoa mwanga. Bila haya, maisha yetu kama wakristo huwa na kasoro. Tusiache kusali na kufanya matendo mema. Injili yetu inatuambia kwamba tukifanya haya tutapokea kuendana na kipimo tulichotoa, naye Bwana atatubariki hivyo hivyo. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni