Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Januari 19, 2021

Jumanne, Januari 19, 2021,
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 6: 10-20;
Zab 111: 1-2, 4-5, 9-10;
Mk 2: 23-28


YESU NA SABATO!

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo katika wimbo wa katikati tunakutana na maneno yasemayo “Bwana analikumbuka Agano lake milele. Zaburi hii inasisitiza juu ya ukweli wa Mwenyezi Mungu katika kutimiza ahadi zake. Itafikia mahali tutafikiria kwamba Mwenyezi Mungu kasahau Agano lake lakini utashangaa kwamba atakuja tu kuitekeleza ahadi yake.

Ndivyo ilivyotokea kwa wana wa Israeli wakiwa utumwani Misri au Babuloni-ilifikia mahali wakafikrii kwamba Mungu ndio kawasahau lakini Bwana alirudi kulikumbuka agano lake. Zaburi hii inatumika kutilia mkazo ujumbe wa somo la kwanza unaotusisitizia kuwa imara kwani hakika Mungu hajasahau ahadi zake. Kama kuna alichoahidi hakika atatekeleza. Kama kuna alichoahidi labda wakati wa ubatizo wetu au ndoa au kupitia kanisa hakika atatekeleza. Lakini itafikia wakati tutaona kana kwamba Mungu ametusahau-hatimizi tena ahadi yake. Sisi tunapaswa kuendelea kuwa imara na kujua kwamba Mungu hadanganyi.

Kwenye somo la injili, tunakutana na Yesu akitangaza hadharani kwamba Sabato ipo ili imsaidie mwanadamu. Yoyote yale yaliyopo kwenye imani yetu kwa kiasi fulani lazima yamsaidie mwanadamu. Anatoa mfano wa Daudi aliyediriki hata kula ile mikate mitakatifu iliyowekwa hekaluni na hii ilitumika na makuhani tu. Lakini Daudi alijaribu hata kuila si kwa kujivuna au kwa kiburi bali kwa sababu alikuwa na hitaji na njaa na Bwana akamsikiliza wala hakumwadhibu kwa kosa hili. Daudi alifanya tendo hili kiimani japokuwa lilikuwa tofauti na taratibu. Na Mungu akamsikiliza.

Ndivyo ilivyo na kwetu pia. Mungu ni mwenye upendo, huangalia nia zetu. Yeye sio kama robot ambayo ikishafanyiwa program hii, haibadiliki, yeye ni mwenye upendo mkubwa. Hivyo tujitahidi kutakatifuza nia zetu. Tuwe na upendo kwa wenzetu pia katika kufuata sheria. Baadhi yetu tunatabia ya kujipangia program kali na kuishia kuwa kama robot na kukosa upendo kabisa. Tunawanyima wenzetu hata nafasi ya kuongea nao, tunajiona kuwa bize, ukimwambia mwenzako aje muda huu akichelewa kidogo unakuta kwamba amekosa kila tu.Tusifanye hivi, pawepo na upendo. Tuache kujifanya kuwa roboti. Sisi ni wanadamu.

Maoni


Ingia utoe maoni