Jumatatu, Januari 11, 2021
Jumatatu, 11/01/ 2021,
Juma la 1 la Mwaka
Ebr 1: 1-6;
Zab 97:1-2.6-7.9
Mk 1: 14-20.
WITO WA MUNGU UNADAI UKARIMU.
Kutubu na kuiamini Injili
Huu ndio ujumbe Yesu anaoanza nao mahubiri yake kwa watu. Hii ndio habari njema anayotangaza Yesu. Yohane Mbatizaji alianza mahubiri yake kwa ujumbe huu huu wa kutubu. Kutubu na kumwamini Yesu kuna umuhimu mkubwa sana maishani. Dhambi hutufungia milango ya neema, hutufanya tushindwe kufurahia msaada wa Mungu hapa ulimwenguni.
Tangu mwanzo wa ulimwengu, Dhambi hutoa kifungo kikali sana. Na mwanadamu amekuwa mdhaifu akiangushwa na shetani kila siku-na kwa namna hii amejifungia milango ya neema za Mwenyezi Mungu. Mlango wa neema tutaufungua kwa kutubu. Katika ujumbe wake kwa makanisa saba ya kitabu cha Ufunuo, ujumbe anaoutoa kwa kanisa lililo na dhambi kama la Sardis ni kutubu. Kutubu ni kujisafisha, kujinawisha tena upya. Unapotubu, ndipo roho wa Bwana naye anarudi kwako, anakuja na kufanya maskani kwako.
Kutubu ndiko kulikotegemewa kuliokoe kanisa la Sardis. Sisi Ndugu zangu tusiache kutubu. Tutajipatia faida kubwa kwa njia ya kutubu, tutaweza kupambana na dhambi za kila siku zinazotuandama kwa njia ya kutubu na maisha yetu kuimarika na kuwa bora zaidi. Mwanadamu hawezi kukataa na kusema hana dhambi. Na dhambi kwa kiasi kikubwa zinamuangusha sana. Atakapotubu ndipo atakapoweza kufurahia mapato ya neema na msaada toka kwa Mwenyezi Mungu.
Akina Daudi walipotubu mbele ya Mwenyezi Mungu, walijiondolea adhabu kubwa waliyokuwa wamepangiwa. Mungu alikuwa amekwishapanga mlolongo wa adhabu lakini alipotubu tu aliweza kuondolewa mlolongo ule. Sisi tusiache kutubu.
Kwenye somo la kwanza tunakutana na ujumbe kwamba kwa nyakati hizi, Bwana ameamua kuzungumza nasi kwa njia ya Mwana wake wa pekee aliyemjulisha siri nyingi kwa ajili ya wanadamu, ili wanadamu wapate kuzifahamu. Siri mojawapo ni kwamba ni lazima tutubu na kuiamini injili. Hii ndio siri kuu itakayotuwezesha kupata wokovu kwani ulimwenguni tunakaa kwenye mazingira magumu yenye kuvutia dhambi kiurahisi. Sisi tushike ujumbe huu vyemae
Maoni
Ingia utoe maoni