Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Januari 09, 2021

Jumamosi, Januari 09, 2021,
Juma baada ya Epifania

1 Yoh 5:14-21;
Zab 149: 1-6,9;
Yn 3:22-30.

KUBAKI DAIMA KWAKULITAZAMA FUMBO LA NOELI

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo katika injili yetu tunakutana na Yohane akikiri waziwazi kwamba yeye sio Masiha na kwamba yeye ni lazima azidi kushuka na Yesu kupanda. Anatambua nafasi yake kama mpambe, kama anayekuja kuandaa njia kwa ajili ya mkuu wake.

Ama kweli Yohane alijitambua na kujikubali na kuipenda nafasi hii yake kama mpambe tu wa Bwana Yesu. Ni wachache wenye ujasiri wa namna hii. Wengi wetu hatuko tayari kujitambulisha kama mke au mume wa mtu fulani, au kama mfanyakazi wa mtu fulani kwa sababu ya kufikiri kwamba tukifanya hivyo tunajidhalilisha. Na mara nyingi tumeishia kuingilia maamuzi yaliyo juu yetu na tukaishia kuharibu. Na mbaya zaidi tupo ambao tumeona aibu hata kujitambulisha kama wafuasi wa Bwana. Tukafika maeneo fulani tukaona aibu hata kufanya ishara ya msalaba, au kuvaa hata msalaba au hata kusali.

Yote haya yanatokana na ukosefu wa kujitambua, ndio maana tunamuonea hata Mungu aibu. Ndio maana tumeingilia hata maamuzi ya wakubwa zetu, na ndio maana tumewakana hata wazazi, waalimu, dini, wake na waume zetu. Baadhi yetu tumeishia kugombania madaraka yasiyo yetu kutokana na kutokujitambua na kukubali hali yetu. Kila mmoja wetu amwombe Mungu ili basi aweze kujitambua na kufanya yampasayo.

Somo la kwanza linatueleza kwamba ikiwa tutaomba chochote ambacho kinaendana na matakwa ya Bwana hakika tutakipokea. Wengi wetu tunasali bila kupata kwa sababu tunaomba vilivyo kinyume na matakwa ya Bwana. Tunaomba ili tukawe mabosi; tuwatawale wengine. Wengine tunaomba vitu ambavyo tunajua hatuna uwezo wa kuvifanya lakini tunangangania. Yote haya ni ukosefu wa kujitambua. Tutambue hali yetu nasi hakika tutaweza kumpendezesha Bwana.

Maoni


Ingia utoe maoni