Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Januari 08, 2021

January 8, 2021.
------------------------------------------------
IJUMAA, Baada ya Epifania

1 Yn 5:5-13;
Zab 147: 12-15, 19-20;
Lk 5:12-16.

HAKUNA ASIYE NA THAMANI MBELE YA YESU!

Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo.
Usikubali sifa zikutawale; usitawaliwe na Sifa.

Injili yetu ya leo yatuambia kwamba Yesu alikuwa akitenda miujiza mikubwa. Tendo hili linamfanya afurahiwe na wengi na kupata umaarufu sana. Alionekana kama 'superstar'. Lakini yeye cha ajabu ni kwamba haruhusu hizi sifa zimkamate, mara moja anaamua kutenga muda wake na kwenda kusali lengo likiwa ni kulinda kazi yake na mafanikio yake. Kwa namna hii aliweza kumshinda shetani aliyetaka kuivamia kazi yake, aliyashinda majivuno, akashinda ubwetekaji na uzembe wowote kwa sababu alithamini kusali.

Sisi tutambue kwamba wengi tunashindwa kuyatunza mafanikio yetu, tunaruhusu shetani aingilie ndani kirahisi. Tunaruhusu tutawaliwe na umaarufu. Sisi tuwe kama Yesu. Ukijiona unafanikiwa na kusifiwa na wengi, jua kwamba shetani yupo karibu na ni lazima tumpinge kwa nguvu zote. Tusiruhusu mafanikio yalete majivuno. Tuyafunike zaidi kwa nguvu ya sala na kwa kufunga zaidi.

Somo la kwanza linatueleza kwamba awezaye kuishinda dunia ni yule aaminiye Yesu kuwa mwana wa Mungu. Yeye anashuhudiwa kwanza na maji na damu. Hivi vinaashiria sadaka na kujitoa kwa ajili ya wengine. Kwa maji yaliyotoka ubavuni mwake, yaliashiria maji ya ubatizo ambayo ndiyo yaliyotutakasa na damu ndiyo iliyotupatanisha na Baba kwa kutufutia lile kosa letu la Mwanzo la wazazi wetu na dhambi zetu zote. Kwa njia ya Roho, yeye hutupatia moto ambao hututakatifuza na kutufanya watoto wapendwa wa Bwana. Yesu ndiye mwenye kututendea yote haya.

Hakika tukimuamini hatutashindwa na ulimwengu bali sisi tutaweza kuushinda huu ulimwengu tena kwa kiurahisi tu. Yesu ana kila kitu cha kutufanya tuushinde ulimwengu na kutupeleka mbinguni. Tuzidi kumwamini. Tujiunge naye kwa sala

Maoni


Ingia utoe maoni