Alhamisi, Januari 07, 2021
Alhamisi, Januari 7, 2021.
Juma baada ya Epifania
1 Yoh 4:19 - 5:4;
Zab 72: 1-2, 14-15;
Lk 4: 14-22
YESU, MASIHI WETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo katika somo la kwanza wazo kuu linalosisitizwa ni kwamba hatuwezi kusema kwamba tunampenda Mwenyezi Mungu ikiwa hatumpendi mwenzetu tunayemuona mbele ya macho yetu. Hili linalozungumzwa na Yohane ni kweli.
Mara nyingi tunatabia ya kujionesha. Tunajidai kwenda kutoa misaada kwa watu wa mbali wakati wale tunaokaa nao karibu wanahangaika ajabu. Tunatabia ya kutafuta umaarufu, tunatoa pale tu tunapoonekana. Haya yote ni lazima tujirekebishe, tabia za namna hii zinawafanya wengi waumie na kutelekezwa.
Tusitegemee kwamba watu wa mbali watafahamu matatizo ya maskini waliokaribu yetu kuliko sisi. Sisi ndio tunaofahamu na hakika tuwasaidie. Tupambane pia na tabia za uvivu-kweli tukishaanza kumsaidia mwenzetu, kuna kasumba ya kuchoka kwa haraka kutokana na uvivu. Hatuwezi kumsaidia mwenye shida kila siku bila ya kuchoka au kuanza kumsumanga. Yote haya ni shetani tunayepaswa kupambana naye katika maisha yetu ya kujitolea. Yanayo turudisha nyuma na vitu kama hivi. Sisi tupambane navyo.
Katika injili, Yesu anakataliwa na watu wa kijijini kwake. Sababu zinazotolewa zinaendana na familia yake-kwamba alitoka familia ya kawaida tu, Baba yake na Mama yake walifahamika kama watu wasiokuwa na jipya. Hivyo walikataa kumpokea. Tabia hii iliwafanya wasipate nafasi ya kufanyiwa miujiza toka kwa Yesu kama ilivyokuwa kwa miji mingine. Halafu hata Yesu hakuchagua mitume wake miongoni mwa hawa watu wa kijijini mwake.
Ndugu zangu, Yesu huvutiwa na wanyenyekevu. Hufurahia kukaa mahali ambapo amekaribishwa na kujisikia nyumbani. Aliamua kujionesha kwa wachungaji kwa sababu wachungaji walikuwa rahisi kumpokea. Sisi tusiache kuwa wanyenyekevu mbele ya Yesu. Tujifungue, tumpokee naye atakuja kwetu. Majivuno humfukuza Yesu. Nasi pia tunaalikwa kuwa na unyenyekevu wa kuweza kumvutia kila mmoja wetu. Tujiweke kwa namna ambayo kila mmoja wetu anaweza kuja kwetu na kukaribishwa. Tusijione kuwa mashuhuri sana au wakuu sana kiasi kwamba tunashindwa kumkaribisha mwenzetu. Tuache tabia hizi. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni