Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Januari 06, 2021

Januari 6 2021.
------------------------------------------------
JUMATANO, BAADA YA EPIFANIA

1 Yn 4:11-18;
Zab 72: 1-2, 10, 12-13;
Mk 6: 45-52.

KUTULIZA DHORUBA KATIKA MAISHA YETU!

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la injili. Hapa tunakutana na wanafunzi wakiwa wenyewe kwenye bahari wakitaabika na dhoruba kali na mawimbi. Na majaribu haya wanayapata tena baada ya kuona muujiza mkubwa wa Bwana Yesu, muujiza wa kuwalisha watu maelfu.

Baada ya muujiza huu tu wanadumbukia kwenye majaribu ya kuteswa na mawimbi baharini kiasi cha kukata tamaa. Ule muujiza walioonyeshwa na Yesu wa kuweza kuwalisha maelfu ya watu ungalipaswa kuwaongezea imani kipindi hiki cha majaribu baharini. Lakini wao inaonekana hawakusaidiwa na ule muujiza, waliishia kuogopa na kusahau kila kitu na hata Yesu alipofika kwao, walishindwa kumtambua wakafikiri kwamba ni lipepo limewajia kuwaongezea shida tena.

Sisi nasi ndugu zangu huwa tunaonyweshwa miujiza na Bwana kila siku. Upo wakati Mungu anakusaidia. Sasa, ikifika wakati ule wa shida au majaribu, tunapaswa kusaidiwa na yale matumaini tuliyoonywesha na Bwana kipindi kile cha msaada. Tukiruhusu kutawaliwa na vipindi vya matatizo, tutashindwa kusaidika, hata Bwana akija kwetu tutamchanganya tudhanie kwamba bado ni mzimu tu.

Basi tuzidi kumuita Bwana hata wakati wa matatizo, tusitumie nguvu zetu tu kama hawa wanafunzi. Akija kwetu hata muda wa kufanya kitu unapungua. Wengi tunafanya vitu kwa muda mrefu kama hawa wanafunzi kwa sababu ya ukosefu wa Bwana.

Kwenye somo la kwanza tunaelezwa kwamba Mungu ni upendo nasi yatupasa kuwapenda wenzetu. Binadamu ni viumbe vya Mungu. Hata kama sisi tutavichukia, Mungu atazidi kuvipenda. Hatuwezi kumzuia Mungu asivipende. Tuache tabia za kuwachukia watu bila sababu, au tabia za kuwatazama wenzetu kwa macho ya hasira na chuki. Hata tukiwaangalia kwa macho ya chuki vipi, hakika watazidi kupendwa tu na Bwana. Bwana hawezi kuwaacha na hatutaweza kuzuia riziki zao. Tuache macho yenye chuki kwa wenzetu.
-------------------------

Maoni


Ingia utoe maoni