Jumamosi, Disemba 26, 2020
Desemba 26, 2020
JUMAMOSI, OKTAVA YA NOELI
Sikukuu ya Mt. Stefano, Shahidi wa kwanza
Somo la 1: Mdo 6:8-10, 7:54-59 Mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume analinganisha jinsi Stefano, “akijazwa na neema na nguvu, aliyefanya mambo makuu na ishara kati ya watu,” anaonekana kuwakera watu na hivyo akauwawa.
Wimbo wa katikati: Zab 30: 3-4,6,8,16-17 mikononi mwako Ee Bwana naiweka roho yangu. Wewe ni mwamba wangu. Ninaomba mwanga wako umwangazie mtumishi wako. Niokoe kwa mwanga wako.
Injili: Mt. 10:17-22 Yesu anatabiri jinsi wafuasi wake watakavyo onewa na anawaambia wasiwe na wasi wasi. “atakaye vumilia mpaka mwisho ataokoka kifo”.
------------------------------------------------
YESU NI SABABU. NI LENGO LETU
Shahidi wa Habari Njema ya Mtoto Yesu:
Mt. Stefano alikuwa miongoni mwa wale mashemasi saba katika kanisa la mwanzo waliosimikwa kwa lengo la kuwasaidia mitume. Tunaona katika somo la kwanza kwamba yeye alikuwa mkristo hodari, aliyekuwa amejawa na Roho Mtakatifu na aliielewa vizuri injili. Yeye alitambua kwamba lengo la ujio wa Yesu lilikuwa kuwafunulia na kuwaelewesha watu juu ya Baba (Yn 17:6).
Alitaka watu wamjue Mungu kikamilifu na wamwabudu katika utakatifu, uhuru, unyenyekevu na Amani (Lk 1:74). Na alitambua kwamba ni Yesu tu, tunayeendelea kufurahia
kuzaliwa kwake kipindi hiki ndiye awezaye kutufunulia juu ya Baba kwa sababu tulisikia katika injili ya jana kwamba yeye anatoka katika kifua cha baba.
Hivyo, ni yeye tu awezaye kutufunulia juu ya Baba. Mafundisho mengine juu ya Mungu, hata kama ni Torati bado yanamhitaji Yesu ayapatie kibali. Bila Yesu, mafundisho mengine juu ya Mungu hukosa ukamilifu: unakuta yamejawa na mawazo ya uongo na ubinadamu mwingi.
Katika somo la kwanza, tunagundua kwamba Stefano alielewa hili na
kulitetea kikamilifu kwamba ni Yesu tu awezaye kutufundisha juu ya Baba. Wengine wote hawawezi, ndani ya dini yote hamna ispokuwa Yesu. Hivyo, katika somo la kwanza, anawapinga waziwazi wanaopotosha watu wasimwabudu Mungu katika utakatifu, uhuru na Amani. Huu ni utume mgumu na Yesu katika injili anawaonya
kwamba watapata matesho mengi. Watasalitiwa hata na ndugu zao kwani wengi
hawatakubali kuachana na desturi zao na kupokea mafundisho haya kirahisi.
Wengi watataka kuwafundisha mitume kuliko kukubali wao kufundishwa na mitume.
Mungu anaahidi kuwa nao na leo anakuwa upande wa Stefano.
Stefano anakuwa shahidi wa kwanza kwa sababu ya kutetea habari njema inayoletwa na
mtoto Yesu. Nasi kama Stefano, tushuhudie habari njema inayoletwa na Kristo duniani: kumtangaza Mungu kuwa ni nani na kuwafanya watu wamwabudu katika uhuru, Amani na upendo.
Lazima tuzipinge mila na desturi zinazowafanya waamini washindwe kumwabudu Mungu katika uhuru, utakatifu na Amani. Vitu kama ushirikina vinatufanya
tushindwe kumwabudu Mungu katika uhuru na utakatifu. Tuachane na wasiwasi na woga. Baadhi ya wakristo ni watu wa wasiwasi na wemeishia katika kudanganywa.
Unakuta mkristo anakutana na mjusi chumbani mwake halafu anaogopa hata kulala kwenye hicho chumba. Anahamia kwa jirani au lazima atafute mtaalamu wa kumfafanulia maana ya huo mjusi aliyeko ndani ya chumba chake. Vitu hivi vinatutia hofu na kutufanya tusimwabudu Mungu katika uhuru.
Wengine wanakuambia ukitaka biashara yako iende vizuri, usiruhusu wateja kuja kununua chumvi usiku, au wakija kununua chumvi usitamke neno chumvi
watamke neno jingine. Watu wanaamini hivyo. Hivi vyote hutufanya tushindwe kumwabudu Mungu katika utakatifu na uhuru kamili.
Au mwingine anakuambia biashara ili iende hakikisha hufungui biashara kwa kukopesha. Yote haya yanatufanya tushindwe kumwabudu Kristo katika utakatifu.
Wengine wanaamini kwamba utajiri au biashara yako ili iende lazima uwe na tunguli au hirizi mfukoni na kufuata masharti. Habari njema ya Yesu haina masharti hayo, yenyewe hutupatia neema na uhuru wa kweli. Tuepuke kudanganywa, wengi tumekuwa maskini na hata kukosana na ndugu zetu kwa ajili ya kudanganywa. Tuishi injili yetu tuweze kuwa huru.
Maoni
Ingia utoe maoni