Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Disemba 29, 2020

Desemba 29, 2020.
------------------------------------------------

JUMANNE, OKTAVA YA NOELI

Somo la 1: 1Yn 2: 3-11 Yohane anatuambia kwamba hatuwezi kumfahamu Yesu hadi tumeshika amri zake: kumpenda Mungu na jirani.

Wimbo wa katikati: Zab 95: 1-3,5-6 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, tangazeni wokovu wake siku kwa siku na maajabu yake kati ya watu.

Injili: Lk 2: 22-35 Luka anatuambia kuhusu kutolewa kwa mtoto Yesu hekaluni, na Simeon anatabiri kwamba upanga utapenya katika moyo wa Maria Mama yake Yesu.
------------------------------------------------

UWEPO WA MUNGU KATI YETU!

Karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la injili tunakutana na Mzee Simeoni akishangilia baada ya kukutana na Bwana. Anayo kila sababu ya kufurahi kwa sababu ni kitu alichokisubiria kwa maisha yake yote na leo amekipata. Ameweza kukutana ya yule aliyetegemeo na mwanga wa mataifa. Hivyo basi aliona maisha yake kukamilika. Aliona kwamba Kristo amemletea mengi sana na hivyo akawa na kila sababu ya kufurahi.

Sisi ndugu zangu tunapaswa kuonesha furaha kama hii ya Simeoni. Tutambue kwamba maisha yetu yanafikia ukamilifu kwa kukutana na Yesu, bila Yesu aliona kupungukiwa. Kukutana na Yesu aliona maisha yake kufikia ukamilifu.

Nasi tunapaswa kuwa na hamu kama hii aliyokuwa nayo Simeoni. Lazima tujione kwamba tumepungukiwa, kwamba bila Yesu hatujafikia ukamilifu bado. Hata tunapokuja kanisani, lazima tuone kwamba bila ile Ekaristi bado hatujakamilika.

Tamaa ya namna hii ndiyo itakayoweza kutubadilisha na kutufanya tuone umuhimu wa Yesu maishani mwetu. Mioyo yetu lazima iandaliwe kama wa simeoni, yeye muda wote alikuwa akienda hekaluni akitegemea kwamba labda atakutana naye. Nasi tuwe na maandalizi ya namna hii pia na hakika tutaweza kuiona nguvu ya Kristo maishani mwetu.

Basi ndugu zangu tusisahau kujitayarisha kwa mapokezi ya Bwana wetu na hasa kwa kuwapenda wenzetu kama Yohane anavyosisitiza kwenye somo la kwanza. Tuache kuwachukia watu bila sababu, wao ni viumbe vitakatifu vya Mungu. Tutembee nao, tuwasaidie katika shida, na tuondoe chuki kwa wengine bila sababu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni