Jumanne, Disemba 22, 2020
Jumanne, Desemba 22, 2020,
Juma la 4 la Majilio
1 Sam 1: 24-28;
1 Sam 2: 1, 4-8;
Lk 1: 46-56
MSIFU MUNGU KILA WAKATI!
Ndugu zangu karibuni katika adihimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Katika tafakari ya masomo yetu ya leo, tunakutana na kina Mama wawili waliojaa furaha na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa matendo makuu aliyowatendea.
Somo la kwanza lamhusu mama yake Samweli. Yeye alionja ugumu na uchungu wa kukaa bila mtoto, huku akisengenywa na kudharauliwa na wanawake wenzake. Bwana alimtendea makuu na leo amekuja kushukuru wema wa Bwana aliomtendea.
Mama Maria na yeye amejaa shukrani kwa Mungu kwa makuu aliyomtendea ya kuwa Mama wa Masiha. Hii ni nafasi iliyotamaniwa na kila mwanamama ndani ya taifa la Israeli. Sasa kiajabu inamuangukia Maria na yeye hana cha kufanya bali ni kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Moyo wa shukrani unapingana na uchoyo. Ukiwa mchoyo kwa Mungu, tusipotoa shukrani kwake ndio sababu zetu sisi kuanguka ndugu zangu na kushindwa kulinda kile kidogo tulichokipata. Ukweli ni kwamba Mama yake Samweli aliongezewa zaidi watoto wengine kwa kitendo chake cha yeye kuja na kumtolea Mungu shukrani. Mungu alimfungulia milango ya fanaka tele. Na Mama Maria alifunguliwa milango ya fanaka tele kwa kitendo chake cha kutoa sala hii ya shukrani.
Sisi tuyalinde mafanikio yetu kwa moyo wa shukrani zaidi. Mafanikio yasituletee kujivuna au kumkana Mungu au kuacha kutambua nafasi yake kwetu. Mafanikio yanalindwa kwa njia ya sala. Kuacha kusali kwa sababu ya kiwewe kiletwacho na mafanikio imetunyima mengi.
Leo ni siku ya kuchunguza yote niliyoacha kumrudishia Mungu kama shukrani na kumpatia nafasi yake. Nitambue kwamba hali yangu imezidi kuwa mbaya kutokana na kutojitambua kwamba ninapaswa kumrudishia Mwenyezi Mungu shukrani. Kumbuka ukipiga magoti na kuomba kitu, ukipata usisahau kutoa shukrani kwa Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni