Alhamisi, Disemba 17, 2020
Alhamisi, Desemba 17, 2020,
Juma la 3 la Majilio
Mwa 49: 2, 8-10;
Zab 71: 1-4, 7-8, 17;
Mt 1: 1-17
JE, UNATAMBUA MPANGO WA MUNGU JUU YAKO?
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati tunakutana na zaburi yenye kutabiri utawala wa Masiha. Utawala huu unaelezewa kama utawala wa kutamaniwa na wanaitamani ile haki itakayopatikana ndani yake. Maskini na wanaoonewa wanategemewa kufurahia zaidi. Katika viongozi wote wa Israeli, hakuna mahali popote ambapo palitokea utimilifu wa utawala huu.
Masiha tu ndiye tumtegemeaye afanye ukamilifu wa utawala huu. Somo la Injili linamuonesha Masiha, yaani Yesu Kristo alitoka katika uzao wa Abrahamu. Sisi wakristo ni wazao wapya wa Abrahamu. Tulipatiwa hadhi hii kuu na Yesu. Hivyo tutambue hadhi yetu. Tujaribu kuuiga utawala wa Yesu.
Kama utawala huu ulivyotamaniwa kwa hamu, sisi tuishi tunu za utawala huu hasa wale tulio viongozi. Tuwahudumie vizuri wale tunaowaongoza, wajisikie nyumbani, wakituambia shida zao tuwajibu, tuwatie moyo, tusiwajibu kwa kashfa. Kwenye kutoa hukumu tuhakikishe tunabakia upande wa haki, tusijiunge na wenye fedha kukakandamiza wanyonge au kuwatelekeza. Wao wapewe nafasi ya pekee kabisa.
Katika somo la kwanza, inadhihirishwa kwamba kabila la Yuda ambalo ndilo lililomtoa Masiha lilipatiwa baraka maalum na Baba yao yaani Yakobo. Sisi tutambue kwamba tabia njema na baraka tuzipokeazo duniani ni za muhimu sana. Hizi zitabariki hata uzao wetu kwa siku zijazo. Tujitahidi pia kuwa na tabia njema na kujitunza katika tabia hizi njema. Wengi wetu tunapoteza mengi kwa sababu ya kutojitunza, Mama Maria aliweza kuubariki ulimwengu kwa sababu ya kujitunza. Sisi tusiache kujitunza naye Bwana atatubariki. Tusiwe watu wa kukusanya laana toka kwa wenzetu tunaoishi nao hapa duniani. Tuwahudumie wenzetu nasi tutajikuanyia baraka. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Bertha Nyigu
Asante kwa neno hili la MunguIngia utoe maoni