Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Disemba 16, 2020

Jumatano, Desemba 16, 2020,
Juma la 3 la Majilio


Is 45: 6-8, 18-25;
Isa 45: 6-8, 18-25;
Zab 85: 8, 9-13;
Lk 7: 19-23.

JE, NI YESU UNAMSUBIRIA?

Katika Injili ya Luka leo, Yohane Mbatizaji anawaagiza Wafuasi wamuulize Yesu, “Je, ni yeye ajaye au tumtazamie mwingine?” Hili pia ni swali la muhimu sana lililopo ndani kabisa mwa moyo wa kila mmoja wetu, je ni ‘wewe’ ninayekusubiri, ‘ambaye’ nimekusubiri maisha yangu yote? Na Yesu anakuwa nashauku ya kumjibu Yohane na sisi pia, Yesu anatoa jibu hili: “Nendeni mkamwambie Yohane mliyo yaona ninyi na kusikia, vipofu wanapona, viwete wanatembea, wakoma wanaponywa, viziwi wanapata kusikia na waliokufa wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema”. Kwa maneno mengine, Yesu anatujibu sisi akisema,”mimi ndiye unayemsubiri, ambaye amekuja kukuokoa na kufanya mambo yote mapya”

Injili hii inatualika tuyaseme maswali yetu yaliyo ndani kabisa mwa mioyo yetu, na kwa nguvu kabisa ya unyenyekevu kama wa Yohane, tumuulize Yesu kilichopo ndani kabisa mwa mioyo yetu. Yesu anatamani kututimizia hamu ya mioyo yetu, atafanya hivyo tuu kama sisi tutaonesha unyenyekevu wa kumwomba, kwasababu Yesu haingilii uhuru wa mwanadamu. Ni jukumu letu tuchague lililo sahihi tutumie uhuru wetu vizuri na kumwomba yeye, kwani kwa hakika yupo tayari kutimiza tunayotaka kumwomba.

Tunaomba kipindi hiki cha Majilio kiwe kipindi cha kumtambua Yesu, ukweli, ambao tunautafuta. Tuzamishe mawazo yetu kwake tuweze kusikia yale yote anayotaka kutuambia Bwana wetu.

Sala:
Bwana, nisaidie katika kipindi hiki cha majilio kuendelea kuandaa moyo wangu. Nisaidie nisikie maneno yako na yote unayotaka kusema nami. Naomba nikufuate katika yote na kati ya yote nikutambue wewe kama Mwokozi wa maisha yangu, Mkombozi ambaye nimemsubiria katika maisha yangu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni