Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Disemba 04, 2020

Ijumaa, Desemba 4, 2020
Juma la 1 la majilio.

Isa. 29:17-24;
Zab 27:1,4,13-14;
Mt 9:27-31


KUTAMBUA UPOFU WETU!

Karibuni ndugu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza tunaendelea kukutana na maneno ya matumaini kwamba mambo yanakuja kuwa mazuri, wale waliodharaulika watapata wakati mzuri wa kufurahia, kupata matumaini na mambo kusonga mbele vyema zaidi.

Wana wa Israeli wanaahidiwa ujio wa atakayekuja kuwasaidia, hata wale waliokosa ufahamu na viwete watapata tu msaada. Sisi katika maisha yetu tukazanie Bwana aje kwetu, akija kwetu ndio sababu ya matumaini na furaha yote. Wengi tuna wasiwasi, shinda na matatizo kwa sababu hatuko na Bwana, tunapaswa kumualika Bwana akae kwetu. Bwana hukaribishwa kwa njia ya sala, sakramenti na kutenda matendo mema. Wengi tunashindwa mengi kwa sababu hatuko na Bwana.

Wale vipofu wanaweza kupata uponyaji kwa sababu ya uwepo wao pamoja na Bwana. Walipomtafuta Yesu na kuja kwao, walipata kuona, na shida zote zikawaishia. Sisi tumwombe Bwana aje kwetu, atufundishe kuona, atufundishe namna ya kuongoza maisha yetu, atufungue macho yetu yapate kuona. Wengi tunaufahamu mdogo, tunakosea kwa mengi; maamuzi yetu ya kimaisha tunayapanga vibaya na mwishowe tunakosea vibaya sana.

Bwana akija kwetu hakika hatutakosea kiasi hiki; hatutatumia fedha zetu vibaya kwa kutapanya ovyo, hatutashindwa kirahisi kwenye kuchagua yale ya muhimu kwa maisha yetu. Bwana atatupatia ufahamu wa kutosha tupate kuona mambo yaliyo ya muhimu. Wengi hatujayajua bado yaliyo muhimu na ndio maana maisha yetu ni duni. Tumwombe Bwana aje kwetu na kutufundisha hekima, atufunulie pia juu ya uzuri wa kuishi maisha ya adili, juu ya uzuri uliopo kwenye kusaidia wenzetu, juu ya uzuri uliopo pale tunapopokea sakramenti na kuungama. Wengi wetu ni vipofu wa mambo haya-hatujui furaha yake. Bwana atuwezeshe kuona furaha ya maisha bila dhambi na maisha ya kukaa na Bwana.

Maoni


Ingia utoe maoni