Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Disemba 02, 2020

Desemba 2, 2020.
------------------------------------------------
JUMATANO, JUMA LA 1 LA MAJILIO

Somo la 1: Isa 25:6-10 Isaya anaona maono kuhusu furaha ya milele mbinguni wakati njaa ya kila mwanadamu itakapo shibishwa, na Bwana Mungu atafuta machozi yote kutoka katika kila uso.

Wimbo wa Katikati: Zab 22:1-6 Bwana ndiye mchungaji wetu. Katika malisho ya majani mabichi, hutupa pumziko.

Injili: Mt 15:29-37 Yesu anawaponya viwete na wagonjwa wengi, anawalisha umati kwa mikate na samaki, kimiujiza.
------------------------------------------------

NJAA YA KUMPATA MUNGU

Ndugu zangu katika Kristo karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu. Masomo ya leo yanatuongoza vizuri katika kipindi hichi cha majilio. Na leo tunasikia kwamba Masiha ajaye atatuandalia karamu. Watu wa Yuda walikabiliwa na umaskini, ukame na vita vilivyowafanya wakabiliwe na upungufu wa chakula mara kwa mara. Hivyo wengi walizoea kula chakula duni na baadhi ya nyakati hakikuwatosheleza. Karamu zilipatikana kwa matajiri na wafalme tu na maskini hawakuruhusiwa kuhudhuria. Lakini katika somo la kwanza, Isaya anawatabiria ujio wa wakati ambapo Bwana atawaandalia karamu. Karamu hii haitakuwa na ubaguzi au kutindikiwa.

Katika injili ya leo, tunaona Kristo anawaonjesha mfano wa hii karamu isiyo na ubaguzi au kutindikiwa kwani makutano wanakula hadi kusaza. Katika kitabu cha Ufunuo 19:9 Mwanakondoo (Yesu) atatuandalia karamu na watakaoingia kwenye karamu ni wale ambao hawakuona aibu kumwungama. Huko Mwanakondoo atafuta giza lote, kilio, kifo na kuomboleza (Ufu 22:3-5) kama Isaya alivyotabiri katika somo la kwanza.

Ujumbe huu ututie moyo ili tuusubirie mwisho wetu kwa matumaini. Tumuombe Yesu atuongoze tuweze kumshuhudia kwa maisha yetu, kukwepa ubaguzi wa aina yeyote anapo tukirimia mapaji yake. Tuwe tayari kushirikisha watu wake. Ili mwishowe tukutane naye katika karamu ya Mwanakondoo,

Maoni


Ingia utoe maoni